Feb 09, 2018 07:59 UTC
  • Ufuska uliopindukia watikisa Bunge la Uingereza

Kamati moja ya Bunge la Uingereza imetoa ripoti ya kutisha kuhusu ufuska mkubwa na utovu wa maadili ulioko baina ya wabunge wa nchi hiyo na kutoa wito wa kubuniwa taratibu maalumu za kuwaadhibu wahalifu ikiwa ni pamoja na kusimamisha ubunge wao au kufukuzwa kabisa bungeni.

Ripoti hiyo ambayo sehemu yake ilifichuliwa kwenye vyombo vya habari Alkhamisi ya jana imesema kuwa, zaidi ya nusu ya wafanyakazi wa Bunge la Uingereza wameshuhudia au wamefanyiwa ukatikli wa kingono na mienendo ya utovu wa maadili ya wabunge.

Ripoti hiyo inasema kuwa, humusi ya wasaidizi wa wabunge wa mabunge mawili ya nchi hiyo ni wahanga wa ukatili wa kingono na kwamba, asilimia 75 miongoni mwao hawajaripoti ukatili huo kwa kuogopa kufukuzwa kazi. 

Ripoti hiyo iliyotayarishwa kutokana na uchunguzi wa maoni ya wafanyakazi 1377 wa Bunge la Uingereza, imethibitisha kuwa, nusu ya wahanga wa ukatili huo wa kingono hawana imani na maafisa wa masuala ya nidhamu na kwa msingi huo hawajawasilisha mashtaka yao. 

Michael Fallon amejiuzulu kutokana na kashfa za ufisadi wa kiamaadili

Ripoti hiyo imetayarishwa baada ya ile iliyotolewa mwaka jana kuhusu ufuska na utovu mkubwa wa maadili unaofanyika ndani ya Bunge la Uingereza huko Westminster uliomlazimisha Waziri wa Ulinzi, Michael Fallon na aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Damian Green kujiuzulu nyadhifa zao. 

Gazeti la Times limeripoti kuwa, wabunge 40 kati ya 45 wanaokabiliwa na tuhuma za ufuska na ukatili wa kingono wanatoka chama cha Conservative na wamo katika baraza la mawaziri la nchi hiyo na kwamba majina yao yamo katika orodha iliyopewa jina la 'faili chafu'.    

Maoni