• Safari ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani nchini Misri

Rex W. Tillerson, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani akiwa katika safari yake ya kiduru katika kuzitembelea nchi za eneo, aliwasili jana mjini Cairo, mji mkuu wa Misri.

Kufanya mazungumzo na viongozi wa Misri juu ya ushirikiano wa Washington na Cairo, na kudumisha mawasiliano kuhusiana na masuala muhimu ya kieneo, hususan kadhia ya Palestina na mji wa Quds (Jerusalem) ni miongoni mwa malengo ya safari ya Tellerson nchini Misri. Safari ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani nchini Misri imefanyika katika hali ambayo, hivi sasa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika inakabiliwa na matatizo mengi ya kiuchumi, umasikini, ukosevu wa ajira, ugaidi na mapambano dhidi ya janga hilo. Kuhusiana na uchaguzi wa rais, serikali ya Cairo inakabiliwa na ukosoaji mkubwa hasa kuhusiana na masuala yanayohusiana na haki za binaadamu na uhuru wa kisiasa.

Rex W. Tillerson, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani

Hata kama Misri ina nafasi maalum kwa Washington kutokana na nafasi yake ya kijografia, hususan katika stratijia ya eneo la Mashariki ya Kati, lakini hadi sasa Marekani na Misri bado zina tofauti za kimtazamo kuhusiana na masuala mengi. Suala la uingiliaji wa Washington katika masuala ya ndani ya uchaguzi mkuu ujao nchini Misri, ni miongoni mwa maudhui ambazo kwa mara kadhaa viongoni wa Cairo wamekuwa wakiilalamikia Marekani. Kama ilivyoshuhudiwa hivi karibuni ambapo Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri ilitoa taarifa kuhusiana na ukosoaji wa Seneta John McCain kwa viongozi wa nchi hiyo ya Kiarabu juu ya ukiukaji wa haki za binaadamu na mwenendo wao wa kuwatia mbaroni wagombea wa uchaguzi ujao wa rais. Katika taarifa hiyo Cairo mbali na kupinga ripoti hiyo ya McCain, iliitaja kuwa ya uzushi na isiyo na ukweli wowote.

Picha ya Rais Abdel Fattah el-Sisi wa Misri anayekosolewa kwa kuwakandamiza wapinzani

Suala la Quds Tukufu na hatua ya Rais Donald Trump wa Marekani ya kuutangaza mji huo kuwa mji mkuu wa utawala haramu wa Israel sambamba na kutaka kuhamishwa ubalozi wa Marekani kutoka Tel Aviv kwenda mji huo, ni suala lingine ambalo Washington na Cairo zinahitilafiana pia. Katika uwanja huo, Rais Abdel Fattah el-Sisi alisema, mgogoro wa Palestina na Israel utatatuliwa kwa pande mbili kufanya mazungumzo na Marekani pia kushirikishwa. Licha ya tofauti hizo kwa mtazamo wa Washington, nafasi iliyonayo Misri na kutokana na kupakana kwake na Libya, inaweza kusaidia katika kupatikana amani na utulivu katika nchi za eneo sambamba na kupambana na makundi ya kigaidi. Ukweli ni kwamba, hatua ya Marekani ya kuongeza misaada yake ya kijeshi kwa Misri, inaweza pia kuongeza uingiliaji wake katika eneo la Mashariki ya Kati.

Raia wa Misri wakiandamana kulalamikia maisha magumu

Kwa upande mwingine ni kwamba Washington inafahamu kuwa, ikiwa itafuata siasa za kuitenga Misri, itakuwa imempoteza mmoja wa washirika wake wakongwe katika ulimwengu wa Kiarabu, suala ambalo pia litailazimu Cairo kujikurubisha kwa Russia ambapo kutokana na ushindani mkubwa iliyonayo Moscow katika matukio ya Syria, jambo hilo litakuwa na maana ya kuibuka vikwazo na changamoto zaidi katika siasa za Washington katika eneo la Mashariki ya Kati. Kuhusiana na suala hilo, Robert Stephen Beecroft, balozi wa Marekani mjini Cairo anasema: "Kuongezeka mabadilishano ya kibiashara kati ya Misri na Marekani, kutasaidia kuimarisha ushirikiano wa pande mbili, kwani Cairo ni moja ya washirika wa kistratijia wa Washington." Mwisho wa kunukuu. Alaakullihal, licha ya kwamba safari ya Rex W. Tillerson, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani nchini Misri inatajwa kuwa itakayosaidia kutatuliwa masuala ambayo nchi mbili zinatofautiana kwayo, hata hivyo inaonekana kwamba, tofauti hizo sio za kutatuliwa kirahisi.

Tags

Feb 13, 2018 02:57 UTC
Maoni