• UN: Myanmar haijaandaa mazingira salama ya kurejea nchini Warohingya

Kamishna Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) amesema Myanmar imeshindwa kuandaa mazingira salama ya kuruhusu kurejea kwa khiari nchini humo Waislamu wakimbizi 688,000 Warohingya waliokimbilia nchi jirani ya Bangladesh.

Filippo Grandi jana Jumanne aliuambia mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa, masharti yaliyowekwa ili kuruhusu mchakato bora wa kurejea nchini Myanmar wakimbizi hao hayajatekelezwa, hususan suala la wakimbizi hao kupewa dhamana kuwa haki zao za msingi kama vile uraia zitalindwa mara tu watakaporejea nchini.

Shirika la UNHCR limetangaza kuwa, kufukuzwa kutoka Bangladesh wakimbizi Waislamu wa jamii ya Rohingya na kurejeshwa kwa nguvu nchini Myanmar ni jambo linalotia wasiwasi mkubwa mno.

Wakimbizi Waislamu wa Rohingya

Serikali za Bangladesh na Myanmar pamoja na Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa zilikubaliana hivi karibuni kuanzisha mchakato wa kuwarejesha wakimbizi hao wa Kirohingya huko Burma kwa khiari, zoezi linalotazamiwa kuchukua miaka miwili.

Mbali na malaki kulazimika kuwa wakimbizi, maelfu ya Waislamu wa kabila la Rohingya nchini Myanmar wameuawa na maelfu ya wengine kujeruhiwa tangu kuanza wimbi jipya la mashambulizi ya jeshi na Mabudha wenye misimamo mikali katika mkoa wa Rakhine magharibi mwa nchi hiyo tarehe 25 Agosti mwaka jana hadi sasa.

Tags

Feb 14, 2018 07:25 UTC
Maoni