• Lengo la Marekani nchini Afghanistani sio kupambana na ugaidi

Rais wa zamani wa Afghanistan, Hamid Karzai amesema kuwa, lengo la Marekani katika uwepo wake kijeshi nchini humo, sio kupambana na ugaidi.

Kwa mujibu wa Karzai, uwepo kijeshi wa Marekani nchini Afghanistan si kwa ajili ya kupambana na ugaidi, bali ni kwa malengo ya kukabiliana na washindani wa Washington katika eneo. Sambamba na kusisitiza kwamba, Washington imeigeuza Afghanistan kuwa eneo la kutekelezea mikakati yake katika eneo, ameongeza kuwa ili kupambana na makundi ya wabeba silaha nchini Afghanistan, hakuna haja ya kuwepo kambi zote za kijeshi za Marekani zilizopo hivi sasa nchini humo. Aidha rais huyo wa zamani wa Afghanistan, amesisitiza kuwa Marekani imewadanganya wananchi wa Afghanistan.

Hamid Karzai, rais wa zamani wa Afghanistan

Ukweli ni kwamba kuendelea kushtadi mgogoro na machafuko ya umwagaji damu nchini Afghanistan, kiuhalisia kunabainisha kwamba, Marekani haikupeleka majeshi yake nchini humo kwa ajili ya kuimarisha usalama na amani, bali inafuatilia malengo yake haramu kupitia mgogoro huo ili kuibadili Afghanistan kuwa ngome yake ya kijeshi kwa ajili ya kuwasafirisha magaidi na wanachama wa makundi yenye kuchupa mipaka kuelekea Asia ya Kati hadi kufikia mipaka ya China. Lengo kuu la njama hizo ni kupora vyanzo vya utajiri wa madini na maliasili nyingine za thamani za mataifa ya eneo. Ni kwa kuzingatia nafasi ya kipekee ya kijografia ya Afghanistan, ndio maana Marekani inakusudia kuibadili nchi hiyo kuwa ngome yake ya ujasusi kwa ajili ya kufuatilia nchi kama vile Russia, China, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na mataifa mengine ya eneo ikiwemo pia India.

Askari wa Marekani nchini Afghanistan

Kwa msingi huo si tu kwamba roho za raia wa Afghanistan hazina umuhimu wowote kwa Marekani, bali pia Washington inafanya njama kupitia mgogoro wa Afghanistan, izirubuni nchi za Pakistan na India. Kufuatia hali hiyo, Ismail Khan waziri wa zamani wa nishati na maji wa Afghanistan anasema: "Raia wa Afghanistan walipambana na Urusi ya zamani na kuishinda, ambapo hatimaye wavamizi walilazimika kuondoka katika ardhi ya nchi hii. Hata hivyo baada ya hapo Afghanistan ilivamiwa na mvamizi mwingine kwa jina la Marekani kwa kisingizio cha kudhamini usalama wa nchi hii. Hivyo udhamini huo wa usalama na amani ndani ya nchi hauwezi kufikiwa sambamba na mashambulizi ya kila mara ya Marekani nchini Afghanistan." Mwisho wa kunukuu.

Machafuko nchini Afghanistan

Askari wa Marekani wamekuwa nchini Afghanistan kwa miaka 16 sasa ambapo katika kipindi hicho wamefanya jinai zisizohesabika. Kushambulia vikao vya harusi, kuwaua raia wakiwa maeneo ya kupumzika, kuanzisha jela za kuogofya na kuwatesa wananchi kwa visingizio tofauti, ni baadhi ya jinai za askari hao vamizi wa Marekani, ambapo hata hivyo aghlabu ya jinai zao hazijaakisiwa. Katika uwanja huo, Muhammad Hashem Fasihi, mtaalamu wa masuala ya kisiasa anasema: "Marekani imeigeuza Afghanistan kuwa eneo la kujaribia silaha zake, na hivi sasa eneo zima hususan Afghanistan limekuwa uwanja wa ushindani wa madola yenye nguvu duniani, na madhara ya kadhia hiyo yanawapata moja kwa moja raia wa kawaida wa eneo na Afghanistan." Mwisho wa kunukuu.

Damu zinamwagika kila siku nchini Afghanistan

Alaa kulli hal, wakati Marekani bado inaendelea kutekeleza jinai zake nchini Afghanistan, nafasi ya Umoja wa Mataifa kuhusiana na suala hilo imekuwa ndogo mno, huku ripoti juu ya uharibifu na idadi ya wahanga wa mashambulizi ya kigaidi zikiwa haziwekwi wazi. Hii ni katika hali ambayo raia wa Afghanistan walitaraji kuona Umoja wa Mataifa kama taasisi pekee ya kimataifa iliyo na jukumu la kusimamia amani duniani, ikisaidia kuimarisha usalama na amani nchini humo kwa kushirikiana na nchi za eneo. Kinyume na hali hiyo ni wazi kuwa Marekani itaendelea kuidhibiti kikamilifu Afghanistan na kutekeleza jinai zaidi za kutisha nchini humo.

Tags

Feb 18, 2018 14:00 UTC
Maoni