• Trump angalau ona aibu; mwanafunzi aliyebaki hai Stoneman Douglas amwambia rais wa Marekani

Mwanafunzi wa skuli ya sekondari ya Stoneman Douglas huko Parkland, katika jimbo la Florida nchini Marekani ambayo hivi karibuni ilishuhudia bahari ya damu baada ya kijana wa miaka 19 kuivamia skuli hiyo na kufanya mauaji ya kutisha, amemtaka rais wa Marekani, Donald Trump, aone haya na ajiheshimu.

Televisheni ya al Alam imemnukuu Emma Gonzales, mmoja wanafunzi aliyeokoka katika shambulio hilo la kikatili akimtaka Donald Trump aone aibu kutokana na siasa zake mbovu za kibaguzi na za kuunga mkono umiliki silaha kiholela nchini Marekani.

Mwanafunzi huyo amesema, maafa yote yanayotokana na utumiaji silaha za moto ambayo yanatokea kila siku nchini Marekani yanasababishwa na siasa za rais wa nchi hiyo, Donald Trump ambaye ana uhusiano mzuri na Jumuiya ya Taifa ya Silaha za Moto.

Nduli wa mauaji ya skuli ya sekondari ya Stoneman Douglas huko Parkland, katika jimbo la Florida akiwa chini ya udhibiti wa polisi

 

Amesema, mwaka 2016 timu ya uchaguzi ya Trump iliipa jumuiya hiyo mamilioni ya dola kwa ajili ya kujiimarisha zaidi na amelaani vikali siasa hizo za rais wa Marekani.

Siku chache zilizopita, taasisi ya The Anti-Defamation League ya kulinda haki za raia wa Marekani ilisema kuwa, Jordan Jereb, mkuu wa genge la Republic of Florida lenye chuki na wageni na taasubu za kizungu, alitangaza wazi kuwa Nikolas Cruz, kijana wa miaka 19 aliyefanya umwagaji mkubwa wa damu katika shule ya sekondari ya Stoneman Douglas na kusababisha wimbi la damu shuleni hapo, alikuwa mwanachama wa genge hilo.

Takwimu zinaonesha kuwa, watu wa kawaida nchini Marekani wanamiliki mamilioni ya silaha kiasi kwamba takriban kila familia nchini humo inamiliki silaha japo moja ya moto.

Tags

Feb 19, 2018 03:04 UTC
Maoni