• Korea Kaskazini yaionya Marekani isifanye manuva ya kijeshi na Korea Kusini

Korea Kaskazini imeonya Marekani kuhusiana na kufanya manuva ya pamoja ya kijeshi na Korea Kusini baada ya michezo ya olimpiki ya msimu wa baridi.

Gazeti la chama tawala cha Korea Kaskazini la Rodong Sinmun limeandika uchambuzi katika toleo lake la leo na kueleza kwamba, endapo Marekani itafanya manuva ya kijeshi ya pamoja na Korea Kusini, hatua yake hiyo itakuwa sawa na kumwagia maji ya baridi katika uhusiano ya Korea Mbili ambao umekuwa na muelekeo wa kuboreka katika siku za hivi karibuni.

Aidha gazeti hilo limeandika kuwa, manuva hayo ya kijeshi yatafanyika kwa lengo la kuhitimisha uhusiano wa Korea Mbili baada ya kumalizika mashindano ya olimpiki ya msimu wa baridi. 

Viongozi wa Marekani na Korea Kaskazini

Kadhalika gazeti hilo limeashiria hatari ya kuibuka mzozo katika Peninsula ya Korea na kudai kwamba, manuva hayo ya kijeshi ya Marekani na Korea Kusini yataichochea Korea Kaskazini iamue kufanya majaribio ya nyuklia.

Korea Kaskazini imekuwa ikiilaumu Marekani kutokana na hatua yake ya kutuma zana nyingi za kijeshi, idadi kubwa ya askari wake na kufanya maneva mbalimbali ya kijeshi katika Rasi ya Korea suala ambalo kwa mujibu wa Pyongyang linashadidisha mgogoro katika eneo hilo.  

Viongozi wa Korea Kaskazini wanainyooshea kidole cha lawama serikali ya Marekani wakisema kuwa, ndio chanzo cha mzozo unaotokoka katika eneo hilo kutokana na hatua zake za kiuhasama dhidi ya nchi hiyo.

Feb 19, 2018 07:50 UTC
Maoni