• Wamarekani waitisha maandamano ya kupinga uhuru wa kubeba bunduki

Familia za waliouawa katika tukio la kigaidi la ufyatuaji risasi katika shule moja ya jimbo la Florida nchini Marekani wanapanga kufanya maandamano makubwa ya kitaifa kupinga sheria ya uhuru wa raia kubeba bunduki.

Wazazi na familia za waliouawa katika tukio hilo la kigaidi wamesema, wanapanga kufanya maandamano makubwa tarehe 24 Machi mwaka huu kulalamikia sheria ya uhuru wa raia kubebe bunduki nchini humo.

Bunduki katika duka moja nchini Marekani. Silaha zinauzwa kama bidhaa nyingine tu nchini Marekani.

Kampeni ya maandamano hayo imepewa jina la "Maandamano kwa ajili ya uhai wetu" huku makundi mbali mbali nchini humo yakiwa katika mkakati wa kushinikiza kuwepo sheria za kudhibiti umiliki wa silaha miongoni mwa raia.

Itakumbukwa kuwa, Jumatano iliyopita, watu wasiopungua 17 waliuawa na makumi ya wengine walijeruhiwa baada ya kijana mmoja gaidi mwenye umri wa miaka 19 kufyatua risasi katika skuli moja ya sekondari ya eneo la Parkland katika jimbo la Florida nchini Marekani.

Kwa mujibu wa polisi, gaidi huyo ambaye ameshakamtawa na ambaye amejulikana kwa jina la Nikolas Cruz, alikuwa mwanafunzi wa zamani wa shule hiyo lakini alifukuzwa kwa sababu za utovu wa nidhamu ambao haujabainishwa ni wa aina gani. Kijana huyo mzungu ana itikadi kali za ubaguzi wa rangi, chuki dhidi ya Waislamu mbali na kuwa mfuasi sugu wa Rais Donald Trump wa nchi hiyo.

Wanafunzi wa skuli ya sekondani ya Stoneman Douglas huko Florida Marekani wakiliwazana baada ya gaidi huyo kufanya mauaji ya kikatili na kusababisha bahari ya damu shuleni hapo

 

Kila siku makumi ya Wamarekani huuawa au kujeruhiwa katika matukio mbali mbali ya ufatuaji risasi kiholela. Kwa mujjibu wa takwimu, Marekani ndio nchi ambayo raia wake wanamiliki idadi kubwa zaidi ya bundiki kiasi kwamba kati ya kila watu 100, watu 90 wanamiliki bunduki.

Lakini pamoja na kuwepo hali hiyo, mashirika ya kutegeneza na kuuza silaha yana ushawishi mkubwa katika chama tawala cha Republican na pia chama cha upinzani cha Democrat; hivyo ni vigumu kwa bunge la nchi hiyo kupitisha sheria zozote za kudhibiti au kuzuia raia kumiliki silaha.

Tags

Feb 19, 2018 15:31 UTC
Maoni