• Kijana mwenye chuki na Uislamu nchini Uingereza awatishia kifo Waislamu

Ikiwa ni katika kuendelea chuki dhidi ya Uislamu (Islamophobia) nchini Uingereza na hujuma dhidi ya misikiti na waumini wa Kiislamu wanaotekeleza ibada ya Sala, kijana mmoja wa nchi hiyo ametishia kwamba atawaua Waislamu.

Gazeti la Daily Star la Uingereza limeandika katika ripoti yake kwamba, kijana mmoja mdogo Muingereza mwenye umri wa miaka 17 amesambaza picha zake akiwa ameshika bunduki na kando yake kukiwa na matangazo ya Kinazi na kutishia kwamba, atawaua Waislamu.

Gazeti hilo linaripoti zaidi kwa kuandika kwamba, kijana huyo mwenye misimamo ya kufurutu ada sio mtu wa kwanza nchini Uingereza kuwatishia kifo Waislamu wa nchi hiyo.

Takwimu zinaonyesha kuwa, uhalifu unaotokana na chuki dhidi ya Waislamu na hujuma dhidi ya misikiti nchini Uingereza uliongezeka maradufu katika mwaka uliopita wa 2017 ikilinganishwa na mwaka wa kabla yake. 

Chuki dhidi ya Uislamu

Hayo yanajiri katika hali ambayo, Waislamu barani Ulaya hususan Uingereza, katika miaka ya hivi karibuni wameanzisha kampeni za kuwafahamisha wasiokuwa Waislamu mafundisho ya Uislamu ili kuondoa fikra potofu miongoni mwao kuhusiana na dini hii.

Jumapili ya juzi Jeremy Corbyn kiongozi wa chama cha Leba cha nchini Uingereza alisema kuwa, chuki dhidi ya Uislamu ni tatizo kwa jamii ya nchi hiyo ya bara Ulaya na kwamba, dini ya Uislamu ni nembo ya amani na kujitolea.

Jeremy Corbyn  alisema hayo katika msikiti wa Finsbury  kaskazini mwa London katika kampeni ya nchi nzima nchini Uingereza inayoendeshwa na Waislamu na ambayo inajulikana kwa jina la "Tembelea Msikiti Wangu" na kubainisha kwamba, uhalifu unaofanywa kwa sababu ya chuki dhidi ya Uislamu unatia aibu.

Tags

Feb 20, 2018 04:32 UTC
Maoni