• Mkutano wa Valdai na sisitizo la Iran la kutatuliwa kwa amani migogoro ya kikanda

Siasa za nje za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zimesimama juu ya msingi wa kutoingilia mambo ya ndani ya nchi nyingine na kuheshimu haki ya kujitawala na mamlaka ya nchi za Mashariki ya Kati.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Dokta Muhammad Javad Zarif ambaye alikuwa akihutubia mkutano wa Valdai mjini Moscow unaojadili hali ya eneo la Mashariki ya Kati. Amesema utatuzi wa migogoro ya eneo la Mashariki ya Kati hususan huko Syria unahitajia hatua za kisiasa na kuongeza kuwa: "Hatua ya Marekani ya kutumia makundi ya waasi kupigana kwa niaba yake katika eneo hilo ni jambo hatari sana."

Iran daima imekuwa ikifanya jitihada kubwa za kuhakikisha kwamba, migogoro ya eneo la Mashariki ya Kati inatatuliwa kwa njia za kisiasa. Hali ya sasa ya Syria na Iraq na ushindi mtawalia dhidi ya Daesh na makundi mengine ya kigaidi katika nchi hizo ni matokeo ya ushirikiano wa kikanda uliosimamiwa na Iran na Russia na nchi nyingine waitifaki. Hata hivyo na licha ya kushindwa kundi la kigaidi la Daesh huko Iraq na Syria lakini bado kunashuhudiwa changamoto ya ugaidi, na kwa sasa magaidi waliosalia wanahama au wanahamishwa kutoka Iraq na Syria na kuelekea katika maeneo ya karibu na mipaka ya Iran na Russia huko Afghanistan.

Muhammad Javad Zarif

Kushindwa kwa Daesh na makundi mengine ya kigaidi huko Iraq na Syria kumetoa pigo na kuzitia hasara kubwa nchi za kibeberu kama Marekani na utawala haramu wa Israel. Hii ni kwa sababu Daesh ni sehemu ya nyenzo za utekelezaji wa mpango wa Marekani wa kuvuruga amani na usalama katika Mashariki ya Kati na kuzigawa baadhi ya nchi za eneo hilo kwa shabaha ya kulinda usalama wa Israel. Hata hivyo mpango huo umefeli na kuvuruga mlingano na mahesabu ya Washington na washirika wake yaani utawala haramu wa Israel na utawala wa Kifalme wa Saudi Arabia. 

Kabla ya kushiriki katika mkutano wa Valdai huko Russia, Dokta Muhammad Javad Zarif alihutubia mkutano wa Usalama wa Munich nchini Ujerumani ambako aliashiria tukio la kutunguliwa ndege ya kijeshi ya Israel huko Syria siku chache zilizopita na kusema: "Tukio hilo limezidi kuvunja ngano kwamba, utawala wa Kizayuni haushindiki."

Mwanasiasa na jenerali mstaafu wa jeshi la Saudi Arabia, Anwar Ashqi pia amesema kuhusu kutunguliwa ndege ya F-16 ya Israel huko Syria kwamba: "Sasa kanuni za mchezo katika Mashariki ya Kati zimebadilika."

Mkutano wa Valdai

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti ya Nur anasema, lengo la kueneza ugaidi kunakofanywa na nchi kama Marekani ni kutaka kuzifanya nchi walengwa kuwa medani na tonge rahisi kwa nchi vamizi. Anasema: Uvamizi wa Marekani katika nchi za Iraq na Afghanistan na kuanzisha makundi ya kigaidi katika nchi hizo na Mashariki ya Kati kwa ujumla vinafanyika ili kuzishughulisha nchi hizo na matatizo ya ugaidi. Wachambuzi hao wanasisitiza kuwa, Marekani inafanya hayo yote ili kuziondoa madarakani serikali na tawala zinazopinga matakwa yake kwa upande mmoja na wakati huo huo kuchafua sura safi ya dini ya Uislamu.      

Feb 20, 2018 14:26 UTC
Maoni