• UN yaendelea kuandamwa na kashfa za kijinsia

Mkurugenzi mtendaji wa mpango wa kudhibiti UKIMWI wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa, naibu wa mkuu wa ofisi hiyo amelazimika kujiuzulu kutokana na tuhuma za kimaadili zinazomkabili.

Shirika la habari la Reuters limemnukuu Michel Sidibé akisema hayo jana Ijumaa na kuongeza kuwa, Luiz Loures, naibu wa mkuu wa ofisi hiyo ya kudhibiti Ukimwi ya Umoja wa Mataifa amekumbwa na tuhuma za kuwa na uhusiano haramu wa kijinsia, hivyo ameamua kujiuzulu.

Michel Sidibé amesema, Luiz Loures ameamua kutorefusha muda wa kuhudumu kwenye ofisi hiyo ambao unamalizika mwisho mwa mwezi ujao wa Machi.

 

Ripoti hiyo imeongeza kuwa, huyu ni afisa wa pili wa ngazi za juu wa Umoja wa Mataifa kujiuzulu kutokana na tuhuma za kimaadili katika kipindi cha siku chache zilizopita.

Siku chache zilizopita, Justin Forsyth, naibu wa mkuu wa ofisi ya utekelezaji ya Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF alilazimika kujiuzulu baada ya kukumbwa na tuhuma za kuwa na uhusiano haramu wa kijinsia katika miaka ya baina ya 2011 na 2015 na baadhi ya wafanyakazi wa kike wa tawi la Uingereza la taasisi ya kuokoa watoto.

Kabla ya hapo, Umoja wa Mataifa ulikuwa umetangaza mwezi huu wa Februari 2018 kwamba, katika kipindi cha miezi mitatu ya mwishoni mwa mwaka 2017, maafisa wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa, Taasisi (Institutes), Mifuko (Funds) na Mipango (Programs) ya umoja huo pamoja na mashirika yake yalikumbwa na tuhuma 40 za udhalilishaji wa kijinsia. 

Tags

Feb 24, 2018 00:50 UTC
Maoni