• Mazungumzo ya Netanyahu na Trump sambamba na kuanza manuva makubwa ya kijeshi ya Marekani na Israel

Rais Donald Trump wa Marekani ameunga mkono katika mazungumzo yake na Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala ghasibu wa Israel misimamo ya utawala huo katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu na kusema kwamba, yumkini akashiriki katika hafla ya ufunguzi wa ubalozi wa Washington huko Beitul-Muqaddas.

Trump amesema kuwa, ushirikiano wa Marekani na Israel haujawahi kuwa mzuri na wenye ukuruba namna hii kama ilivyo hivi sasa. Waziri Mkuu wa Israel ameelekea Washington kwa ajili ya kushiriki katika mkutano wa kila mwaka wa Kamati ya Marekani na Israel ya Masuala ya Umma (AIPAC) na kukutana na Rais wa Marekani.

Safari ya Benjamin Netanyahu huko Washington inafanyika katika hali ambayo, yameanza manuva ya kijeshi ya pamoja ya Israel na Marekani katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina.

Duru za Kizayuni zimetangaza kuwa, askari 2500 wa marekani na 2000 wa Israel wanashiriki katika manuva hayo ya kijeshi ya pamoja. Manuva hayo ya kijeshi yanatajwa kuwa makubwa kabisa ya pamoja kuwahi kufanywa na Marekani na Israel. Uungaji mkono wa kisiasa wa Washington kwa Israel kuhusiana na Beitul-Muqaddas na ushirikiano wa kijeshi wa pande mbili ni sawa na Marekani kuipa idhini Israel ya kuanzisha duru mpya ya hatua za kupenda vita na propaganda za kisiasa kwa ajili ya kuwatwisha Wapalestina na nchi za Kiarabu siasa zake za kupenda kujitanua.

AIPAC

Mick Napier mwanaharakati wa Kiscotland anaashiria misimamo ya Marekani hususan ya serikali ya Trump ya kuiunga mkono Israel na kusisitiza kwamba, moja ya sababu kuu za kupanuka wigo wa uvamizi wa Israel katika ardhi za Palestina ni huu uungaji mkono wa Washington.

Katika kipindi cha uongozi wa Trump, uungaji mkono wa Marekani kwa Israel haujaishia katika masuala ya kiuchumi na kisiasa tu, bali wigo wake huo umo katika hali ya kupanuka pia katika uwanja wa ushirikiano wa kijeshi. Uungaji mkono wa Marekani kwa Israel ni siasa za daima za Washingtion ambazo zimekuwa zikipewa kipaumbele na Marais wote wa nchi hiyo wanaoingia katika ikulu ya White House. Baadhi ya Marais hao wakiwa wahudumu wazuri wa Wazayuni wamewashinda wenzao katika hilo; na Rais Donald Trump ni mmoja wa Marais hao.

Hapana shaka kuwa, lobi za Wazayuni zimekuwa na satwa na ushawishi mkubwa katika jamii ya Marekani na Marais wa nchi hiyo wakiwa pamoja na lobi hizo wamekuwa wakisukuma mbele gurudumu la siasa zao za ndani na za kigeni.

Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa Israel

Katika uwanja huo, Rais Trump akitumia mbinu mbalimbali yumo mbioni kuonyesha mapenzi yake maalumu aliyonayo kwa Wazayuni; na matamshi yake ya kujipendekeza katika mazungumzo yake na viongozi wa Israel na katika vikao vya AIPAC yanaunga mkono ukweli huu.

Kushadidi siasa za kujitanua za utawala wa Kizayuni wa Israel kunafanyika katika hali ambayo, Marekani imetangaza katika miaka ya hivi karibu utayari wake wa kuongeza misaada yake isiyo na masharti kwa Israel na kudhamini gharama za Tel Aviv za siasa zake za kujitanua. Kwa mujibu wa makubaliano ya hapo kabla, Israel imekuwa ikipata msaada wa dola bilioni tatu za Kimarekani kila mwaka kutoka kwa serikali ya Washington.

Donald Trump akiwa na Benjamin Netanyahu

Aidha katika makubaliano mapya ambayo yanaweza kutekelezwa katika kipindi cha miaka kumi na kivitendo yamekuwa yakitekelezwa katika kipindi cha uongozi wa Donald Trump, Israel itapokea kifurushi kikubwa zaidi cha misaada ya kijeshi na kiuchumi cha Marekani ambacho hakijawahi kushuhudiwa katika historia ya serikali ya Washington.

Kwa mintarafu hiyo, kiwango cha misaada isiyo na masharti ya Marekani kwa utawala haramu wa Israel kitafikia dola bilioni 42 hadi 45 katika kipindi cha miaka kumi ijayo yaani kuanzia mwaka huu wa 2018 hadi 2028 ambapo sehemu yake kubwa ni misaada ya kijeshi.

Hapana shaka kuwa, uungaji mkono huu wa Marekani kwa utawala wa Kizayuni wa Israel hauna kingine ghairi ya kuongeza kiburi cha utawala huo cha kuendeleza siasa zake za kupenda vita, kujitanua na kushadidisha jinai zake.

Tags

Mar 07, 2018 03:12 UTC
Maoni