Mar 08, 2018 08:19 UTC
  • Kitendawili cha jaribio la mauaji jasusi wa zamani wa Rassia chaanza kuteguliwa?

Polisi ya Uingereza imetangaza kuwa, mtu aliyetaka kumuua afisa wa zamani wa vyombo vya ujasusi vya Russia ambaye baadaye imebainika kuwa alikuwa akiifanyia ujasusi Uingereza, alitumia gesi ya neva.

Polisi ya Uingereza imetangaza kuwa, jasusi wa zamani wa Russia, Sergei Skripal na binti yake, Yulia wanaoishi nchini humo Jumapili iliyopita walishambuliwa kwa gesi ya neva wakiwa katika duka moja kubwa kwenye mji wa Salisbury huko kusini magharibi mwa jiji la London. Wawili hao walikutwa wamepoteza fahamu katika benchi na hali yao ya kiafya inaripoti kuwa ni mbaya sana. 

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, Boris Johnson amesema nchi hiyo itatoa jibu kali kwa upande wowote wa kigeni uliohusika katika jaribio hilo la kuua kwa kutumia sumu.  

Image Caption

 

Sergei Skripal aliwahi kutumika katika taasisi ya ujasusi ya jeshi la Russia na mwaka 2004 alitiwa nguvuni na vyombo vya ujasusi vya nchi hiyo kwa kudhaniwa kuwa, aliwasaliti wafanyakazi wenzake kwa vyombo vya upelelezi vya Uingereza. Mwaka 2006 Skripal alihukumiwa kifungo cha miaka 13 jela. Hata hivyo mwaka 2010 alipewa hifadhi nchini Uingereza katika makubaliano ya kubadilishana majasusi. 

Sergei Skripal alikiri kuwa aliwasaliti maafisa wa upelelezi wa Rusia kwa Shirika la Ujasusi Nje ya Nchi la Uingereza MI6 mkabala wa kupokea kitita cha fedha. Jasusi huyo wa zamani wa Russia amekuwa akiishi Uingereza tangu mwaka 2010. 

Russia imetangaza kuwa, haina habari yoyote kuhusu sababu ya tukio hilo na yaliyompaya Sergei Skripal lakini imesema kuwa iko tayari kushirikiana na polisi ya Uingereza katika kadhia hiyo.     

Tags

Maoni