• Misimamo ya kupingana ya viongozi wa Marekani kuhusu pendekezo la kufanya mazungumzo na Korea Kaskazini

Baada ya Korea Kaskazini kusema kuwa, kuna uwezekano wa kuondolewa silaha za nyuklia eneo la Korea na kurejeshwa uhusiano wa kawaida na Marekani iwapo itadhaminiwa usalama wake, Dan Coats, Mkuu wa Idara ya Intelejensia ya Marekani amesema ana shaka kuhusiana na mambo hayo yote.

Coats amesema kuwa, mambo yaliyotolewa na serikali ya Marekani kwa ajili ya kuishawishi Korea Kaskazini kuketi kwenye meza ya mazungumzo ni malipo kwa Pyongyang ili iweze kutumia fursa hiyo kwa ajili ya kuimarisha zaidi silaha zilaha zake za nyuklia. Kadhalika ameashiria kwamba, mazungumzo ya namna hiyo hayana matunda yoyote na kwamba Kim Jong-un ni mtu mwenye mahesahu.

Rais Donald Trump wa Marekani amejibu pendekezo la Korea Kaskazini kwa ajili ya kufanya mazungumzo akisema Marekani ipo tayari kufanya mazungumzo na Pyongyang na kwamba, suala hilo litafanyika baada tu ya Korea Kaskazini kuachana na silaha zake za nyuklia. 

Mike Pence, Makamu wa Rais wa Marekani

Kwa upande wake Mike Pence, Makamu wa Rais wa Marekani amesema kuwa machaguo yote kuhusiana na Korea Kaskazini yako mezani na kwamba, Marekani lazima ione hatua za kuelekea upande wa kuangamiza silaha za nyuklia za Korea Kaskazini. 

Wakati huo huo Heather Ann Nauert, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani amesema kuwa, siasa za Washington kuhusu Korea Kaskazini bado hazijabadilika.

Matamshi ya kupingana ya viongozi wa Marekani kuhusiana na pendekezo la kufanya mazungumzo na Pyongyang yametolewa sambamba na kutangazwa vikwazo vipya dhidi ya nchi hiyo kwa kisingizio cha kuuliwa ndugu wa Kiongozi wa Korea Kaskazini yaani Kim Jong-nam aliyeuawa na watu wasiojulikana nchini Malaysia.

Dan Coats, Mkuu wa Idara ya Intelejensia nchini Marekani 

Pyongyang imejibu misimamo na matamshi hayo ya viongozi wa Marekani kwa kusema kuwa, mazungumzo na Washington yanawezekana pale kutakapokuwepo mazingira ya usawa baina ya pande mbili na kwamba, kamwe haitaachana na miradi ya kutengeneza makombora ya balestiki na silaha za nyuklia. Vilevile Korea Kaskazini imewasha tena mtambo wake wa nyuklia katika eneo la Yangbyon na kuanza kuzalisha tena plutoniumu kwa ajili ya sihala za nyuklia. Hatua hiyo imetajwa na weledi wa mambo kuwa ni maneva ya kisiasa ambayo pamoja na mambo mengine ina lengo la kuzidisha mashinikizo ya kufanikisha mchakato wa kuondoa mivutano katika peninsula ya Korea.

Weledi wa masuala ya kisiasa wanasema kuwa, kwa sasa Korea Kaskazini imefungua njia ya udiplomasia na kwamba suala hilo linaonekana waziwazi, kwani hadi miezi michache iliyopita hali ya mambo ilikuwa tete baina ya pande hizo mbili kiasi cha kuzungumziwa uwezekano wa kufanyika mashambulizi ya kijeshi.

Silaha za nyuklia za Korea Kaskazini zinazoinyima usingizi Marekani

Kwa mantiki hiyo fursa ya udiplomasia ni lazima itumiwe vizuri sambamba na kuchukuliwa maamuzi chanya kwa kuzingatia pia maslahi ya eneo la Peninsula ya Korea. Pamoja na hayo inaonekana kuwa, White House haiko tayari kwa ajili ya suala hilo. Kuhusiana na kadhia hiyo, John O. Brennan, mkuu wa zamani wa Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) amesema kuwa, ni wazi kwamba Rais Donald Trump hayuko tayari kushughulikia masuala  kama lile la Korea Kaskazini.

Misimamo ya kugongana ya viongozi wa Marekani kuhusiana na pendekezo la kufanya mazungumzo na Pyongyang imedhihirisha waziwazi na kuzidisha tofauti zilizopo miongoni mwa viongozi hao, na kwa kutilia maanani hali hiyo, itakuwa vigumu sana kwa ikulu ya Rais wa Marekani, White House kuchukua maamuzi muhimu ya kimataifa.

Tags

Mar 08, 2018 11:46 UTC
Maoni