Mar 14, 2018 07:53 UTC
  • Korea Kusini: Russia isitutupe mkono katika juhudi za kufungua mahusiano na Korea Kaskazini

Serikali ya Korea Kusini, kupitia Mshauri wa Masuala ya Usalama wa Taifa wa nchi hiyo ameitaka Russia kuiunga mkono Seoul kwa ajili ya kupatikana mahusiano mema na viongozi wa Korea Kaskazini.

Chung Eui-Yong, ameyasema hayo alipokutana na Sargey Lavrov, Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia mjini Moscow, na kuongeza kuwa, kuimarishwa mawasiliano na viongozi wa Korea Kaskazini ni nukta muhimu katika historia ya eneo la Rasi ya Korea na kwamba Russia haitakiwi kuitupa mkono Korea Kusini katika kadhia iliyoratibiwa ya kuwakutanisha pamoja viongozi wa Korea mbili na kadhalika kufanikisha suala la kukutana viongozi wa Korea Kaskazini na Marekani.

Chung Eui-Yong, kulia alipokutana na Lavrov

Kadhalika Chung Eui-Yong amewasilisha pongezi kutoka kwa Rais Moon Jae in wa Korea Kusini kutokana na nafasi chanya ya Rais Vladimir Putin wa Russia katika suala zima la kutatua mzozo wa eneo la Peninsula ya Korea. Mshauri wa Masuala ya Usalama wa Taifa wa Korea Kusini, aliwasili mjini Moscow, Jumatatu kwa ajili ya kufanya mazungumzo na viongozi wa nchi hiyo. Itakumbukwa kuwa, tarehe saba ya mwezi huu ofisi ya rais wa Korea Kusini ilitangaza kuwa, viongozi wa Korea mbili watakutana mwishoni mwa mwezi wa Aprili mwaka huu katika kikao cha kihistoria katika eneo lisilo la kijeshi la Panmunjom ambalo lipo katika mpaka wa nchi hizo.

Chung Eui-Yong, alipokutana na Kim Jong-un mjini Pyongyang siku kadhaa zilizopita

Mahusiano kati ya Pyongyang na Seoul yamekuwa yakiboreka tangu kulipojiri mazungumzo ya pande mbili kwa ajili ya kuishawishi Korea Kaskazini ishiriki katika michuano ya msimu wa baridi kali nchini Korea Kusini. Tangu wakati huo, wajumbe wa pande mbili wameendeleza mawasiliano kati yao na kupelekea hivi karibuni Rais Moon Jae in wa Korea Kusini kumtuma mjumbe wake maalumu mjini Pyongyang kwa ajili ya kukutana na viongozi wa nchi hiyo akiwemo Kim Jong-un, Kiongozi wa Korea Kaskazini.

 

Tags

Maoni