Mar 20, 2018 15:56 UTC
  • Zimwi la Gaddafi lamuandama Sarkozy wa Ufaransa; azuiliwa

Rais wa zamani wa Ufaransa Nicolas Sarkozy, anazuiliwa na polisi ya mjini Paris, kwa ajili ya kusailiwa kuhusu tuhuma za kufadhiliwa na Libya katika uchaguzi wa mwaka 2007.

Idara ya Mahakama nchini Ufaransa imesema Sarkozy pamoja na Brice Hortefeux, waziri wa zamani na mpambe wa karibu wa rais huyo wa  zamani wa Ufaransa wamekamatwa na kuzuiliwa na vyombo vya usalama hii leo kwa ajili ya uchunguzi.

Ufaransa ilimfungulia kesi ya ufisadi Sarkozy mwaka 2013, kwa madai kwamba alipokea kutoka kwa Muammar Gaddafi, dikteta wa zamani wa Libya kitita cha yuro milioni 50 kinyume cha sheria, kusaidia kampeni zake za uchaguzi wa rais wa mwaka 2007.

Gaddafi na Sarkozy katika Ikulu ya Elysee mjini Paris Disemba 2007

Hali kadhalika huko nyuma Sarkozy alifikishwa mahakamani kujibu tuhuma  kwamba, ushindi wake wa mwaka 2007 ulitokana na msaada wa dola milioni 70 zilizotolewa na Muammar Gaddafi, na fedha nyingine kutoka kwa ajuza tajiri wa Kifaransa Liliane Bettencourt mmiliki wa shirika la vipodozi vya I’Oreal. 

Gazeti la Daily Mail linalochapishwa nchini Uingereza liliwahi kufichua kwamba, dikteta wa zamani wa Libya Muammar Gaddafi aliuliwa na ajenti wa siri wa Ufaransa kwa amri ya Sarkozy, ili kumzuia asije akafichua mahusiano yao endapo angesailiwa. 

Tags

Maoni