• Makumi wauawa katika shambulizi la Daesh mjini Kabul, Afghanistan

Kwa akali watu 29 wameuawa huku makumi ya wengine wakijeruhiwa katika shambulizi la kigaidi la Daesh (ISIS) lililolenga mkusanyiko wa watu waliokuwa wakiadhimisha sikukuu ya Nowruz, kuanza mwaka mpya wa 1397 Hijria Shamsia, katika mji mkuu wa Afghanistan, Kabul.

Habari zinasema shambulizi hilo la leo Jumatano limetokea katika eneo la Karte Sakhi, karibu na Hospitali ya Ali Abad, pambizoni mwa Chuo Kikuu cha Kabul, ambapo watu 52 wamejeruhiwa.

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Afghanistan  imesema aghalabu ya waliouawa katika hujuma hiyo ya kigaidi ni Waislamu wa madhehebu ya Shia, waliokuwa wamekusanyika karibu na Haram ya Sakhi kwa ajili ya kushiriki marasimu ya Nowruz.

Mashuhuda wanasema gaidi aliyekuwa amejifunga mada za miripuko alikimbia na kujilipua katika Haram ya Sakhi, baada ya kugunduliwa na polisi. Genge la kigaidi na kitakfiri la Daesh (ISIS) limetangaza kuhusika na shambulizi hilo.

Moshi ukifuka angani kutoka eneo la mripuko mjini Kabul

Hapo jana, raia watatu waliuawa baada ya gari lililokuwa limesheheni mabomu kulipuka mjini Kabul, hujuma mbayo Daesh imekiri kuhusika nayo pia.

Wimbi hili la mashambulizi ya kigaidi yanafanyika katika hali ambayo, kumekuweko na mjadala kuhusu uwezekano wa kufanyika mazungumzo ya moja kwa moja kati ya serikali na wapiganaji wa Taliban, au kati ya genge hilo la kigaidi na serikali ya Marekani. 

 

Tags

Mar 21, 2018 14:03 UTC
Maoni