Mar 28, 2018 06:50 UTC
  • Lavrov atoa onyo kali kwa nchi za Magharibi

Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Russia amesema kuwa Moscow haitanyamaza kimya mbele ya hatua ya nchi za Magharibi ya kuwafukuza wanadiplomasia wa nchi hiyo.

Sergei Lavrov ameyasema hayo akijibu hatua ya pamoja na nchi kadhaa za Ulaya, Marekani, Ukraine, Canada na Australia ya kuwafukuza wanadiplomasia wa Rusia katika nchi hizo. Ameashiria hatua ya baadhi ya nchi kuomba radhi kutokana na kuwafukuza wanadiplomasia wa Russia na kusema hicho ni kielelezo kwamba suala hilo limefanyika kwa mashinikizo makubwa ya Marekani ambayo ndio wenzo unaotumiwa na Washington katika medani ya kimataifa. Russia inaona kuwa, kufukuzwa wanadiplomasia wa nchi hiyo katika nchi kadhaa za Magharibi ni ishara kwamba, nchi zinazojitegemea dunia ni chache sana. 

Wakati huo huo mwakilishi mmoja wa Bunge la Ulaya ametahadharisha kuhusu uwezekano wa kuharibika zaidi uhusiano wa nchi za Magharibi na Moscow na kusema: "Hatua ya kuwafukuza wanadiplomasia wa Russia katika nchi za Magharibi bila ya kuwa na ushahidi wowote wa kuhusika Moscow katika faili la Skripal, inautumbukiza uhusiano wa Magharibi na Russia katika mgogoro mkubwa."

Trump VS Putin

unapotazama taathira kubwa na zinazoendea kupanuka za kufukuzwa wanadiplomasia wa Rusia katika baadhi ya nchi za Magharibi tunaweza kusema kuwa, suala hilo halina mfano katika upeo wa kimataifa.

Hadi sasa nchi 24 za Magharibi zimewafukuza wanadiplomasia wa Russia na idadi hiyo inajumuisha wanadiplomsia 60 waliofukuzwa nchini Marekani hadi nchi kama Finland na Latvia zilizofukuza mwanadiplomasia mmoja tu. Wanadiplomasia 151 wa Russia wamefukuzwa katika nchi hizo na sasa Shirika la Kijeshi la Nchi za Nagharibi (NATO) nalo limeingia katika mpambano huo wa kidiplomasia. Inatazamiwa kuwa taasisi nyingine kadhaa za Kimagharibi pia zitafuata nyayo na kujiunga na mkondo huo. Kwa utaratibu huo idadi ya wanachama wa ujumbe wa Russia katika shirika la NATO itapungua kutoka 30 hadi 20. Kisingizio kinachotumiwa na nchi za Magharibi katika kadhia hii ni madai yaliyotolewa na Uingereza kwamba, Russia ilihusika na jaribio la kumua kwa sumu jasusi wake wa amani, Sergei Skripal na binti yake, Yulia katika eneo la Salisbury huko kusini mwa London. Moscow inakanusha vikali madai hayo.

Jasusi wa zamani Sergei Skripal na binti yake, Yulia

Mtaalamu wa Kirussia, Dmitry Igorchenkov anasema: "Faili la Skripal kama lilivyokuwa lile la Litvinenko kabla yake ni sehemu ya vita vya Marekani, Uingerea na NATO dhidi ya Russia vyenye lengo la kuifanya Moscow itengwe katika nyanja za kisiasa na kijeshi." Inaonekana kuwa nchi za Magharibi zinataka kutumia vibaya madai ya kupewa sumu Skripal kwa shabaha ya kuiwekea Ruussia mashinikizo makubwa ya kimataifa na hatimaye kuilazimisha Moscow ilegeze misimamo yake katika baadhi ya mambo. Kwa sasa takwa kubwa zaidi la nchi za Magharibi kwa Moscow ni kujiondoa katika mgogoro wa mashariki mwa Ukraine na kuacha kuwaunga mkono wanaotaka kujitenga mashariki mwa nchi hiyo, na vilevile kurejesha eneo la Crimea kwa serikali ya Ukraine. Eneo hilo liliunganisha na ardhi ya Russia mwaka 2014 baada ya kura ya maoni iliyofanyika Februari mwaka huo. Wakati huo huo nchi za Magharibi zinaitaka Moscow ibadili misimamo na nafasi yake katika mgogoro wa Syria.

Pamoja na hayo yote inaonekana kuwa, ni jambo lililo mbali kwamba Russia itakubaliana na matakwa hayo ya nchi za Magharibi. Hivyo inatazamiwa kuwa, Moscow pia itajibu mapigo na kulipiza kisasi kwa kuwatimua wanadiplomasia wa nchi za Magharibi. Kwani viongozi wa Kremlini wanaelewa vyema kwamba, kulegeza kamba mbele ya Wamagharibi kutapelekea kuzidi matakwa yao  na kuzidishwa hujuma dhidi ya Russia na si vinginevyo.   

Tags

Maoni