Mar 31, 2018 14:44 UTC
  • Jibu madhubuti la Russia kwa hatua ya nchi za Umoja wa Ulaya

Serikali ya Russia ilitangaza jana Ijumaa kuwa itawafukuza wanadiplomasia 59 wa nchi 23 tofauti walioko nchini humo. Uamuzi huo wa Moscow umechukuliwa kujibu hatua ya nchi hizo ya kuwafukuza kwa mpigo wanadiplomasia wa Russia. Katika jibu na radiamali yake kwa hatua ya kufukuzwa wanadiplomasia wake, serikali ya Moscow imechukua uamuzi wa kuwafukuza wanadiplomasia 41 wa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya.

Siku ya Alkhamisi ya tarehe 29 Machi, Russia ilianza kutekeleza mchakato wa kujibu mapigo kwa kuwafukuza wanadiplomasia 60 wa Marekani walioko nchini humo pamoja na kuufunga ubalozi mdogo wa nchi hiyo ulioko kwenye mji wa Saint Petresburg. Hatua hiyo iliyochukuliwa na Moscow imekabiliwa na msimamo wa ulegezaji kamba wa baadhi ya nchi za Ulaya. Kufuatia kutolewa tangazo la kufukuzwa wanadiplomasia wa Ujerumani, Heiko Maas, Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo amesema, Berlin inakaribisha kufanyika mazungumzo baina yake na Russia na itafanya juhudi ili kuwa na mustakabali chanya na athirifu katika uhusiano wa nchi mbili. Kwa mtazamo wa mtaalamu wa siasa za Ujerumani Volker Peretz, Umoja wa Ulaya unapaswa kufikia maridhiano na Russia.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Heiko Maas

Tab’an mbali na Ujerumani, viongozi wa Umoja wa Ulaya pia wanakubaliana na suala hilo. Mkuu wa Kamisheni ya Ulaya Jean-Claude Juncker, alitamka hivi karibuni kwamba: licha ya hitilafu kubwa zilizoko baina yao na Russia ni makosa kushughulikia masuala ya usalama wa Ulaya bila ya kutilia maanani nafasi ya Russia. Mgogoro wa hivi sasa wa kidiplomasia kati ya Russia na nchi za Magharibi umeelezwa kuwa ni wa nadra kuwahi kushuhudia tokea enzi za Vita Baridi (ColdWar) hadi wakati huu.

Jengo la ubalozi wa Russia mjini London, Uingereza

Ukweli ni kwamba nchi za Ulaya hazikutarajia kwamba, kama Russia ilivyochukua hatua ya kujibu mapigo kwa Marekani, itaamiliana vivyo hivyo na nchi za Ulaya zilizojiunga na kambi ya Uingereza na Marekani kwa ajili ya kukabiliana na Moscow. Hata hivyo hatua iliyochukuliwa na Russia imekuwa tofauti na vile zilivyodhani nchi za Ulaya, ambazo sasa zimebaki zinababaika na kutapatapa. Pamoja na hayo, nchi wanachama wa EU hazijachukua msimamo mmoja katika kukabiliana na Russia kwa kisingizio cha kadhia ya kupewa sumu Sergei Skripal, jasusi wa zamani wa Moscow nchini Uingereza. Japokuwa nchi nyingi za Umoja wa Ulaya zimechukua msimamo dhidi ya Russia, baadhi ya nchi kama Cyprus, Slovania, Ugiriki na Austria hazikuchukua hatua ya kuwaita nyumbani mabalozi wao walioko mjini Moscow, au kuwatimua mabalozi wa Russia walioko katika nchi zao. Hii ni ishara ya kuwepo hitilafu za mtazamo ndani ya Umoja wa Ulaya kuhusu namna ya kuamiliana na Moscow.

Ndege iliyobeba wanadiplomasia wa Russia waliofukuzwa Uingereza baada ya kuwasili Moscow

Kutokana na mgogoro wa Ukraine, tangu mwaka 2014, uhusiano wa Umoja wa Ulaya na Russia umekuwa ukishuhudia mikwaruzano na kuongezeka ufa wa hitilafu na hatua za kuwekeana vikwazo kati ya pande mbili. Kwa mtazamo wa Moscow, uhusiano wa sasa kati yake na EU unapita kwenye kipindi kigumu. Hivi sasa suala la kuendeleza vikwazo dhidi ya Russia, na katika mduara mpana zaidi, kuendeleza uhusiano na nchi hiyo limesababisha hitilafu na mgawanyiko kati ya nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya. Ni wazi kwamba mgongano huo wa mitazamo ndani ya EU umezusha mfarakano na kukosekana mshikamano katika msimamo unaochukuliwa na umoja huo kuhusiana na Russia.

Sergei Skripal, jasusi wa zamani wa Russia nchini Uingereza

Suala la kupewa sumu Skripal, limeplekea mrengo ulio dhidi ya Russia ndani ya Umoja wa Ulaya kuwa na sauti ya juu zaidi. Hata hivyo kungali kuna baadhi ya nchi wanachama wa EU ambazo zinapinga kuchukuliwa hatua hasi dhidi ya Moscow. Pamoja na yote hayo, msimamo wa Russia wa kuchukua hatua kali kuhusiana na kutimuliwa wanadiplomasia wake katika nchi za Ulaya umeonyesha kuwa nchi hiyo haitowapembejea na kuwaridhia Wamagharibi na kwamba msimamo wa kujibu mapigo ndiyo stratejia kuu ambayo nchi hiyo imeamua kuitumia katika kuamiliana na Magharibi, zikiwemo nchi za Umoja wa Ulaya. Pamoja na yote hayo Moscow inaendelea kusisitiza kila mara kwamba, uwezekano ungalipo wa kutatua hitilafu na kurejesha uhusiano wa pande mbili katika hali ya kawaida…/

 

Tags

Maoni