Apr 18, 2018 04:02 UTC
  • Jeremy Corbyn: Ishambulieni Saudia pia kwa kuwa imetumia silaha za sumu Yemen

Kiongozi wa chama cha Leba nchini Uingereza ametaka kufanywa mashambulizi ya anga kuilenga Saudia kutokana na nchi hiyo ya Kiarabu kutumia mabomu yaliyopigwa marufuku na Umoja wa Mataifa dhidi ya raia wasio na hatia nchini Yemen.

Jeremy Corbyn sambamba na kukosoa vikali uamuzi wa serikali ya Theresa May, Waziri Mkuu wa Uingereza wa kushirikiana na Marekani na Ufaransa katika kuishambulia Syria kwa kisingizio cha kutumiwa silaha za kemikali na kadhalika misimamo ya kukinzana ya waziri mkuu huyo kuhusiana na suala zima la Yemen, amesema kuwa mgogoro wa kibinaadamu unaoshuhudiwa Yemen unatoa idhini ya wazi kwa mataifa mengine kuweza kuishambulia Saudia.

Jeremy Corbyn, Kiongozi wa chama cha Leba nchini Uingeza

Amezidi kufafanua kuwa nchi nyingine zinayo haki ya wazi kabisa kuzishambulia kambi za jeshi la Saudia kutokana na nchi hiyo kutumia mabomu yaliyopigwa marufuku aina ya fosforasi katika kuwalenga raia wa kawaida nchini Yemen. Jeremy Corbyn ameyasema hayo katika kikao cha bunge nchini Uingereza ambapo amemuhutubu Spika wa Bunge, John Bercow na kadhalika Theresa May kwa kusema hadi kufikia mwezi Januari mwaka huu mashirika matatu ya kibinaadamu ya Umoja wa Mataifa yalitoa ripoti kwamba Yemen inakabiliwa na hali mbaya ya kibinaadamu, kwa ajili hiyo tunamuomba Waziri Mkuu Theresa May atuahidi leo kwa kutangaza kukomesha uungaji mkono wa London juu ya mashambulizi ya kinyama ya Saudia dhidi ya Yemen na kadhalika uuzaji silaha wa Uingereza kwa Riyadh.

Mabomu yaliyopigwa marufuku ambayo yanatumiwa na Saudia kuua watu wa Yemen na kuwaacha vilema

Kadhalika kiongozi huyo wa chama cha Leba nchini Uingeza amekosoa pupa ya Waziri Mkuu wa Uingereza katika kuishambulia kijeshi Syria na hivyo ametaka kupitishwa na bunge sheria ambayo itaizuia serikali ya London kufanya mashambulizi ya kijeshi bila ya idhini ya bunge. Theresa May ameendelea kukosolewa vikali na viongozi mbalimbali wa Uingereza kutokana na hatua yake ya kuungana na Marekani katika kuishambulia Syria. 

Tags

Maoni