Apr 18, 2018 07:42 UTC
  • Trump: Mimi ni jasusi zaidi ya gaidi wa US anayezuiliwa Uturuki

Rais Donald Trump amejitokeza na kumkingia kifua Padri mmoja raia wa Marekani aliyepandishwa kizimbani nchini Uturuki hivi karibuni kwa tuhuma za kujihusisha na harakati za kigaidi ndani ya taifa hilo.

Trump amemtaja padri huyo aliyejulikana kwa jina la Andrew Brunson kama 'kiongozi wa kidini mwenye ustaarabu' na ambaye amefunguliwa kesi 'bila sababu zozote'.

Rais huyo wa Marekani amesema, "Eti wanasema yeye ni jasusi, lakini mimi ndio jasusi zaidi yake."

Aprili 16, kesi ya padri huyo ilianza kusikilizwa katika mji wa İzmir magharibi mwa Uturuki ambako kuna kanisa analoliongoza.

Brunson alitiwa mbaroni na maafisa usalama wa Uturuki mwezi Oktoba mwaka 2016 akiwa pamoja na mke wake.

Padri Andrew Brunson raia wa Marekani anayezuiliwa Uturuki

Taarifa iliyotolewa na serikali ya Uturuki inasema kuwa, padri huyo alikuwa akiifanyia kazi harakati ya Fethullah Gülen, mtuhumiwa nambari moja wa jaribio la mapinduzi yaliyofeli ya mwezi Julai mwaka 2016 nchini humo.

Vilevile ametuhumiwa kuwa anashirikiana na chama cha Kikurdi cha PKK ambacho serikali ya Ankara inasema ni kundi la kigaidi. 

Kesi ya Andrew Brunson anayetuhumiwa kufanya ujasusi dhidi ya serikali ya Uturuki itasikilizwa tena Mei 17.

Tags

Maoni