• Kikao cha Baraza la Usalama la UN kuhusu Yemen

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa juzi Jumanne lilikutana kujadili kadhia ya Yemen bila hata ya kuashiria jinai zinazoendelea kufanywa na Saudi Arabia dhidi ya raia wasio na hatia wa nchi hiyo huku vita na mashambulizi ya kinyama ya utawala huo wa kifalme vikiingia katika awamu nyingine.

Kikao hicho kilitosheka kukariri madai ya vyombo vya habari vya madola ya Magharibi kuhusu mgogoro wa Yemen. Katika kikao hicho wawakilishi wa Marekani na Uingereza katika Umoja wa Mataifa walikariri madai kuwa, Iran inawasaida wapiganaji wa harakati ya al Huthi na kusisitiza udharura wa kusimamishwa mashambulizi ya harakati hiyo dhidi ya Saudi Arabia. Madai hayo yametolewa huku mashambulizi ya kinyama ya Saudi Arabia dhidi ya watu wa Yemen yakiendelea kwa miezi 37 sasa. 

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambalo limepoteza hadhi na heshima yake baada ya kupuuzwa na Marekani, Ufaransa na Uingereza zilizoamua kuishambulia Syria bila ya ridhaa cha chombo hicho cha kimataifa, bado linatumiwa kama taasisi ya kuhalalisha na kutimiza malengo ya nchi za kibeberu na limeshindwa kuchukua maamuzi huru kuhusu moja kati ya maafa makubwa zaidi ya binadamu katika dunia ya sasa. Baraza hilo ambalo limekuwa likitoa maazimio kila uchao kuhusu Syria, katika kikao cha juzi lilishindwa hata kutoa taarifa ya kulaani jinai na mauaji yanayofanywa na Saudia huko Yemen. 

Hapa linajitokeza swali kwamba, ni kwa nini basi Baraza la Usalama likakutana kujadili kadhia ya Yemen katika kipindi cha sasa? 

Nikki Haley

Matamshi yaliyotolewa na wawakilishi wa Marekani na Uingereza katika kikao hicho cha Umoja wa Mataifa yameweka wazi zaidi sababu za kuitishwa kwake. Mwakilishi wa Uingereza, Karen Pierce alisema kwamba: "London inalaani kwa sauti kubwa mashambulizi yanayofanywa na wapiganaji wa harakati ya al Huthi huko Yemen dhidi ya maeneo ya kiraia ya Saudi Arabia na vilevile utumiaji wa makombora ya balestiki". Pierce amedai kuwa timu ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa imegundua kwamba katika kipindi cha vikwazo vya silaha vya umoja huo kuliingizwa zana zinazotumiwa kuzalisha makombora nchini Yemen kutokea Iran". Matamshi haya yanaonesha kuwa, lengo la kuitishwa kikao hicho cha Baraza la Usalama kuhusu Yemen ni kuishinikiza harakati ya al Huthi na kusitisha uwezo wake wa makombora ya kijihami na vilevile kutoa tuhuma dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Kwa ujumla tunaweza kusema kuwa, lengo la kikao cha juzi cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ni kuitetea Saudi Arabia kwa sababu Riyadh inawaona wapiganaji wa al Huthi na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kama maadui wake. Kikao hicho kimefanyika wakati vita vya Yemen vimeingia katika awamu mpya; kwani katika upande mmoja kuimarika uwezo wa kujihami wa jeshi na makundi ya kujitolea ya Yemen kumetoa pigo kubwa kwa Saudi Arabia na washirika wake, na katika upande wa pili Saudia na Imarati zimezidisha mashambulizi yao dhidi ya watu wa Yemen ili kufunika na kuficha udhaifu na vipigo mtawalia kutoka kwa wanamapambano wa Yemen. Katika Mkondo huo ndege za kivita za Saudi Arabia zimeendelea kushambulia maeneo mbalimbali ya Yemen na kuua raia wasio na hatia.

Malaika wa Yemen wanaendelea kuuawa bila ya dhambi wala hatia yoyote.

Pamoja na hayo yote kikao cha juzi cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hakikuashiria hata kwa mbali jinai na mauaji yanayoendelea kufanywa na Saudi Arabia dhidi ya raia wa Yemen. La kusikitisha zaidi ni kuwa, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres aliyetembelea Saudia na kukutana na viongozi wa nchi hiyo amekwepa hata kuashiria kwa mbali maafa na mauaji yanayofanywa dhidi ya raia wasio na hatia wa Yemen hususan wanawake na watoto wadogo. Mwenendo huu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na Katibu Mkuu wa umoja huo ni kielelezo cha kuporomoka kwa taasisi hiyo ya kimataifa.       

Apr 19, 2018 03:02 UTC
Maoni