• CNN yafichua: Shambulio dhidi ya Syria lilifanywa bila kuwepo uhakika kama silaha za kemikali zilitumiwa Duma

Ukiwa umepita muda wa chini ya wiki moja tangu Marekani na waitifaki wake waishambulie kijeshi Syria kwa madai ya kufanyika shambulio la silaha za kemikali nchini humo, kanali ya televisheni ya CNN ya nchini Marekani imefichua kuwa nyaraka na ushahidi uliotumiwa kwa ajili ya shambulio hilo ni picha tu na sampuli za vipimo visivyo vya moja kwa moja.

Tovuti ya habari ya CNN imeripoti kuwa: maafisa wa intelijinsia na wa kijeshi wa Marekani wameieleza kanali hiyo ya habari kwamba licha ya vyombo vya intelijinsia kutokuwa na uhakika kama serikali ya Damascus imetumia gesi ya kemikali katika mji wa Duma, rais wa Marekani Donald Trump alitoa amri ya kufanywa shambulio la kijeshi dhidi ya Syria siku ya Jumamosi bila ya kuwepo ushahidi wa kutosha.

Afisa mmoja wa jeshi la Marekani amesema, kwa sababu hiyo iliamuliwa mashambulio hayo yasiwe ya muendelezo na kwamba misimamo ya waitifaki wa Syria ikiwemo Russia nayo pia ilichangia katika kuchukua uamuzi huo.

Mji wa Duma ulioharibiwa kwa vita

Afisa huyo wa jeshi la Marekani amefafanua kuwa kabla ya shambulio la Marekani haikuwezekana kutihibitisha kwamba jeshi la Syria limetumia gesi ya sumu katika mji wa Duma.

CNN imeripoti aidha kwamba, maafisa, hasa wa intelijensia wa Marekani wanasisitiza kuwa sampuli za vipimo zilizopo kuhusiana na kadhia hiyo hazikupatikana moja kwa moja kutoka eneo la tukio bali zilipatikana kimagendo na wala haijulikani hasa zimepatikana kutoka wapi.

Marekani, Ufaransa na Uingereza ziliyashambulia kwa makombora maeneo kadhaa ya Syria kwa madai kuwa jeshi la nchi hiyo lilifanya shambulio la silaha za kemikali katika mji wa Duma ulioko kandokando ya mji mkuu wa nchi hiyo, Damascus.../ 

Tags

Apr 19, 2018 03:03 UTC
Maoni