Apr 22, 2018 02:16 UTC
  • Kuundwa kundi la kuipiga vita Russia katika bunge la Uingereza

Bunge la Uingereza limeunda kundi jipya la kuipiga vita Russia. Kundi hilo lililo dhidi ya Russia katika bunge la Uingereza limeundwa kwa kuwashirikisha wajumbe wa kamati sita wenye ushawishi katika bunge hilo wakiwemo wenyeviti wa kamati za ulinzi, masuala ya nje, fedha na usalama wa taifa. Aidha wajumbe wa kamati nyinginezo kama wa masuala ya ndani, utamaduni, vyombo vya habari na masuala ya dijitali pia wamo katika kundi hilo jipya dhidi ya Russia ndani ya bunge la Uingereza.

Kundi hilo dhidi ya Russia katika bunge la Uingereza lilifanya kikao chake cha kwanza bungeni cha kila mwezi Jumatano iliyopita. Washiriki wa kikao hicho walijaribu kila wawezalo kudhihirisha picha kamili ya vitisho vya Moscow dhidi ya London. Inaonekana kuwa  kundi hilo la kuipiga vita Russia limeasisiwa kama sehemu ya hatua zilizo dhidi ya Russia zinazoendelea kuchukuliwa na Uingereza. Sergei Lavrov Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amebainisha kuwa, si siri tena kwamba uhusiano wa nchi mbili hauko katika hali nzuri, lakini akaongeza kuwa suala hilo halihusiani na mwenendo wa Moscow.

Sergei Lavrov, Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia 

Mikwaruzano kati ya Russia na Uingereza nchi ambazo tangu huko nyuma pia zilikuwa zikihitilafiana pakubwa, hivi sasa imefikia katika marhala tete sana kwa kuzingatia tuhuma na hatua zinazochukuliwa na London dhidi ya Moscow kuhusu kadhia ya jasusi Skripal. Kama anavyobainisha Leonid Rink, mchambuzi wa masuala ya kemikali kwamba Russia haina maslahi yoyote katika kupewa sumu nchini Uingereza Sergei Skripal jasusi wa zamani wa Russia; na katika upande mwingine Russia isingeweza kufanya jambo hilo katika kipindi hiki nyeti yaani cha Mashindano ya Soka ya Kombe la Dunia. 

Leonid Rink, Mchambuzi wa masuala ya kemikali 
 

Serikali ya Kihafidhina ya Uingereza imechukua hatua dhidi ya Russia na au inataraji kuchukua uamuzi kutekeleza hatua zake hizi'; masuala ambayo yatauweka uhusiano baina ya nchi mbili katika mkondo usiorejeleka. Wakati huo huo, Washington na Umoja wa Ulaya pia zimeunga mkono kampeni hiyo ya London dhidi ya Russia. Ni wazi kuwa kadhia ya Skripal sasa imegeuzwa kuwa moja ya changamoto zinazoendelea kati ya Russia na nchi za Magharibi. Hali ya mivutano imeshuhudiwa kushtadi katika miaka ya hivi karibuni katika uhusiano wa Uingereza na Russia huku uhusiano huo ukizidi kuingia dosari kutokana na kuwepo hitilafu pia katika mambo mengine mbalimbali baina ya nchi hizo mbili. Moja ya sababu kuu ya kushuhudiwa hali hii ni kuzuka mgogoro wa Ukraine ambao umezifanya Russia na nchi za Magharibi ikiwemo Uingereza kuhitilafiana kimitazamo. Hasa ikizingatiwa kuwa, hatua ya Michael Fallon, Waziri wa Ulinzi wa Uingereza wa wakati huo ya kutoa vitisho vikubwa mwishoni mwa mwezi Aprili mwaka jana ilikumbwa na majibu makali kutoka kwa Russia. Fallon alisema kuwa London inayo haki ya kuzuia shambulio la adui kwa kutumia silaha za nyuklia.

Michael Fallon , Waziri wa Ulinzi wa wakati huo wa Uingereza 

Russia ilivitaja vitisho hivyo kuwa ni sehemu ya vita vya kisaikolojia vya Magharibi dhidi ya Moscow. Mbali na kadhia hizo zote, kuendelea hitilafu baina ya nchi za Magharibi na Russia kuhusu mgogoro wa Syria hususan baada ya muungano wa pande tatu wa nchi za Magharibi kufanya mashambulio ya makombora dhidi ya Syria kumechangia mizozo yote hiyo. Aidha Uingereza ikiwa nchi mshirika wa kistratejia wa Marekani imepindukia hata nafasi ya Washington katika uwanja huo dhidi ya Russia. London imetangaza kuwa haifurahishwi na mwenendo wa Russia na kudai kuwa uhusiano wa London na Moscow hauwezi kurejea katika mkondo wa kawaida kwa kuzingatia kwamba Russia ingali ina nia ya kuvuruga hali ya mambo katika nchi za Ulaya ikiwemo Ukraine. Pamoja na hayo yote, viongozi wa ngazi ya juu wa Uingereza wanatambua vyema nafasi muhimu sana ya Russia kuhusu masuala ya kimataifa hususan kuhusu mgogoro wa Ukraine na wa Syria; na wanaamini kuwa, juhudi zozote za kukomesha migogoro yote hiyo haziwezi kuzaa matunda bila ya kushirikishwa kikamilifu Russia.

Tags

Maoni