Apr 22, 2018 03:46 UTC
  • Trump aendelea kukosolewa, bunge la Ujerumani lalaani shambulizi la Marekani dhidi ya Syria

Kinyume na serikali ya Ujerumani, bunge la nchi hiyo limelaani shambulizi la Marekani, Ufaransa na Uingereza dhidi ya Syria na kulitaja kuwa ni kukiuka sheria na mikataba ya kimataifa.

Gazeti la Ujerumani la Spiegel limeripoti kwamba wawakilishi wa bunge la nchi hiyo kutoka chama cha Kisoshalisti cha Demokratic na mrengo wa kushoto wamelaani mashambulizi ya nchi tatu hizo dhidi ya Syria. Hii ni katika hali ambayo, Angela Merkel Kansela wa Ujerumani aliitaja waziwazi hujuma hiyo kuwa sahihi.

Matokeo ya uchunguzi wa bunge la Ujerumani, yameonyesha kwamba utumiaji nguvu na mabavu dhidi ya nchi huru tena bila kuwepo kibali cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ni ukiukaji wa wazi wa sheria na mikataba ya kimataifa ambayo inakemea ukatili duniani. Wawakilishi wa bunge la Ujerumani pia wameyataja madai ya kutumiwa na serikali ya Damascus silaha za kemikali eneo la Douma nchini humo kuwa yasiyo na itibari yoyote na kwamba, madai ya kutumiwa silaha hizo za kemikali hayawezi kuwa sababu ya kuishambulia kijeshi nchi huru. 

Hali ilivyokuwa wakati wa kujiri mashambulizi hayo ya hivi karibuni

Marekani, Uingereza na Ufaransa, ziliishambulia kijeshi Syria siku ya Jumamosi iliyopita kwa kisingizio cha matumizi ya silaha za kemikali mjini Douma, eneo la Ghouta Mashariki. Hujuma hizo pamoja na kuwa hazikuwa na taathira yoyote, zimelaaniwa vikali kote duniani ikiwemo ndani ya nchi  hizo vamizi.

Tags

Maoni