Mei 25, 2018 13:59 UTC
  • Baada ya kukataa kukutana na Kim Jong-un, Trump aitaka Pentagon ijiandae kukabiliana na Pyongyang

Rais Donald Trump wa Marekani amelitaka jeshi na Wizara ya Ulinzi ya nchi hiyo (Pentagon) kujiweka tayari kwa ajili ya makabiliano tarajiwa na Korea Kaskazini.

Taarifa za ndani nchini Marekani zinaarifu kwamba baada ya rais huyo kuvunja ratiba ya kukutana na Kim Jong-un wa Korea Kaskazini amefanya mazungumzo na James N. Mattis, Waziri wa Ulinzi na Kamanda Mkuu wa Vikosi vya Jeshi la Marekani ambapo amesisitizia udharura wa kujiweka tayari kijeshi kwa ajili ya kukabiliana na hatua yoyote isiyotarajiwa ya Pyongyang. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Rais Donald Trump pia amezitaarifu serikali za Japan na Korea Kusini kuhusiana na kadhia ya kugawana gharama za operesheni hiyo tarajiwa.

Trump anafikiria chaguo la kijeshi dhidi ya Korea Kaskazini

Wakati huo huo gazeti la New York Times limeandika kuwa, ikulu ya Marekani (White House) inadhania kwamba mashambulizi ya kushtukiza dhidi ya Korea Kaskazini ni chaguo sahihi, lakini ukweli ni kwamba si rahisi kiasi hicho kwa kuwa hatua yoyote ya kijeshi dhidi ya nchi hiyo itasababisha maafa makubwa. Likielezea kuwa, hatua ya kuvunja kikao kilichotarajiwa kufanyika nchini Singapore kati ya Trump na Kim Jong-un itaharibu zaidi mahusiano kuliko ilivyokuwa hapo kabla, limeongeza kwamba serikali ya Trump ambayo mshauri wake ni John R. Bolton, mwenye misimamo mikali ya kupindukia, kwa mara nyingine inafikiria chaguo la kijeshi dhidi ya taifa hilo la Asia.

Baadhi ya makombora ya Korea Kaskazini

Awali ilikuwa imepangwa kwamba viongozi wa Marekani na Korea Kaskazini wangekutana tarehe 12 Juni mwaka huu nchini Singapore, lakini ghafla na bila kutarajiwa Trump alitangaza Alkhamisi ya jana kuvunja kikao hicho. Hii ni katika hali ambayo Pyongyang ilikuwa imekwisha chukua hatua za kuuvutia upande wa pili kwa kusimamisha miradi yake ya nyuklia na majaribio yote ya makombora ya balestiki.

Tags

Maoni