Mei 26, 2018 03:06 UTC
  • Kongresi ya Marekani yampiga marufuku Trump kutangaza vita dhidi ya Iran

Wabunge wa Kongresi ya Marekani wamepasisha kwa kauli moja muswada wa marekebisho ya sheria inayompiga marukufu Rais Donald Trump kutangaza vita dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran bila ridhaa ya Bunge hilo.

Muswada huo wa marekebisho ya Sheria ya Bajeti ya Ulinzi wa Taifa 2019 uliwasilishwa na mbunge wa chama cha upinzani cha Democratic, Keith Maurice Ellison lakini ukapata uungaji mkono hata kutoka kwa wabunge wa chama tawala cha Republican.

Baada ya kupasishwa muswada huo, mbunge huo aliandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter kuwa: "Kupasishwa kwa sheria hiyo kunaonesha wazi namna wananchi wa Marekani na Kongresi haitaki kutangazwa vita dhidi ya Iran, na Bunge la Kongresi limerejesha uwezo na mamlaka yake ya kuidhinisha au kutoidhinisha kutumiwa nguvu za kijeshi."

Hivi karibuni, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mike Pompeo alitangaza kile alichokiita kuwa stratejia mpya ya Washington ya kukabiliana na Iran baada ya nchi hiyo kujitoa kwenye makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, ambapo alitaja masharti 12 ambayo Washington inataka Iran iyatekeleze.

Trump baada ya kusaini dikrii ya kuiondoa US katika makubaliano ya JCPOA

Kongresi imepasisha muswada huo wa marekekebisho ya sheria katika hali ambayo, mwezi uliopita Wabunge wa vyama vya Republican na Democrat nchini Marekani kwa pamoja walitoa radiamali wakimkosoa Rais Donald Trump wa nchi hiyo kwa kuishambulia Syria bila ya kupata idhini ya Kongresi, wakisisitiza kuwa kitendo hicho kilikuwa kinyume cha sheria.

Aidha Trump alipuuza mwito wa wabunge wa chama cha Democrat katika Bunge la Kongresi nchini Marekani waliyomtaka aheshimu na afungamane na mapatano ya nyuklia ya Iran yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezwaji JCPOA.

 

Tags

Maoni