Mei 26, 2018 07:17 UTC
  • Russia: Baada ya kujiondoa JCPOA, Marekani haina haki yoyote kuhusiana na makubaliano hayo

Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia imesisitiza kwamba kitendo cha Marekani kujiondoa katika makubaliano ya nyuklia ya Iran maarufu kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA), kimeiondolea nchi hiyo haki yoyote kuhusiana na makubaliano hayo.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia imetoa ripoti kuhusiana na matokeo ya kikao cha kamisheni ya pamoja ya makubaliano hayo, bila kuwepo upande wowote wa Marekani na kuongeza kwamba washiriki wa kikao hicho cha mjini Vienna, Austria wameonyesha wasi wasi wao mkubwa juu ya hatua ya upande mmoja na isiyo na msingi ya Rais Donald Trump kujiondoa katika mapatano hayo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia Sargey Lavrov

Ujumbe wa Russia katika kikao hicho umesisitiza kwamba hatua hiyo ya Marekani ni ukiukaji  wa wazi wa mapatano hayo ya pande zote katika uga wa kutatua masuala ya nyuklia na pia ukiukaji wa azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililounga mkono mapatano hayo. Kikao cha kamisheni ya pamoja ya makubaliano ya nyuklia ya Iran na ambacho kiliushirikisha upande wa Iran, kilihudhuriwa na nchi tano nyingine wanachama wa makubaliano hayo ya kimataifa ukiwemo pia Umoja wa Ulaya bila kuwepo Marekani.

Siku ambayo makubaliano ya JCPOA yalipofikiwa mwaka 2015

Mapema jana Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Sayyed Abbas Araqchi alisema kuwa, kubakia Iran katika mapatano hayo kutategemea maamuzi ya nchi za Ulaya kuhusu kutoa dhama kwa nchi hii. Hatua ya Trump ya kuiondoa nchi yake katika mapatano hayo ya nyuklia yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA) aliyoichukua tarehe 8 mwezi huu,  imeendelea kukosolewa vikali duniani.

Tags

Maoni