Mei 27, 2018 02:32 UTC
  • Hatua kwa hatua kuelekea Siku ya Kimataifa ya Quds; Marekani mshirika wa jinai za Israel dhidi ya Wapalestina

Siku ya Kimataifa ya Quds ambayo ni siku ya kupazwa duniani sauti ya kudhulumiwa taifa la Palestina na kuchukizwa ulimwengu na utawala katili wa Israel unaoua watoto wadogo, inawadia.

Mwaka huu, Siku ya Kimataifa ya Quds inaadhimishwa katika hali ambayo majeraha makongwe ya Palestina yametoneshwa tena na njama mpya za Marekani dhidi ya taifa hilo madhlumu. Kuhamishwa ubalozi wa Marekani kutoka Tel Aviv hadi mji mtakatifu wa Quds (Jerusalem) kumeifanya Siku ya Quds ya mwaka huu kuwa uwanja wa kudhihirishwa hasira ya walimwengu kuhusiana na kitendo hicho cha jinai cha watawala wa Marekani. Kwa hakika kitendo hicho kimekamilisha jinai zinazotekelezwa na utawala ghasibu wa Israel dhidi ya watu wasio na hatia wa Palestina. Ni wazi kuwa hatua hiyo ya Marekani itakuwa na matokeo mabaya na hatari katika ngazi za kieneo na kimataifa. Ni miaka 70 sasa tokea nchi ya Palestina ivamiwe na kukaliwa kwa mabavu na Beitul Muqaddas pia imekuwa ikikaliwa kwa mabavu na Wazayuni tokea mwaka 1967.

Trump baada ya kutia saini amri ya kuuhamishia ubalozi wa Marekani Quds Tukufu

Katika kipindi hiki chote wananchi wa Palestina ima wamekimbia nchi yao au wanaishi chini ya mateso na ubaguzi mkubwa wa Wazayuni katika maeneo tofauti ya nchi hiyo na hasa katika Ukanda wa Gaza ambapo wanakabiliwa na mzingiro mkubwa wa Wazayuni. Katika mazingira hayo Marekani imeyatangazia wazi mataifa ya eneo na hasa taifa la Palestina kwamba itaendelea kuunga mkono kwa nguvu zake zote ukaliwaji mabavu wa ardhi za Wapalestina na hasa baada ya kuuhamishia ubalozi wake katika mji wa Qud Tukufu kutoka Tel Aviv. Quds ni sehemu muhimu ya utambulisho wa Kiislamu na ni moyo wa ardhi za Palestina. Kwa msingi huo kadhia ya Palestina ni zaidi ya kumiliki ardhi na suala la Palestina kwa hakika ni zaidi ya suala la kuwepo nchi moja ya Kiislamu. Historia inathibitisha kwamba utawala wa Kizayuni kwa kushirikiana kwa karibu na Marekani umekuwa na mipango kabambe na ya muda mrefu kwa ajili ya kudhibiti na kukalia kwa mabavu Quds Tukufu, kupitia mbinu nyingi zikiwemo za kuwafukuza Wapalestina katika ardhi zao za asili, kupora mali zao, kubadilisha muundo wa kijamii wa Quds kwa kujenga vitongoji vya Wazayuni katika eneo hilo na kuivunjia heshima Masjidul Aqsa kwa kuruhusu walowezi wa Kizayuni wenye misimamo mikali kuingia msikitini humo.

Ufunguzi wa ubalozi wa Marekani mjini Quds kinyume na sheria na maazimio ya Baraza la Usalama

Hii ni katika hali ambayo Beitul Muqaddas ni moja ya sehemu tatu tukufu zaidi katika ulimwengu wa Kiislamu. Ni wazi kuwa hatua ya Marekani ya kuhamishia ubalozi wake katika mji huo mtakatifu inavunja na kukiuka moja kwa moja taratibu na sheria za kimataifa, yakiwemo maazimio nambari 478 lililopitishwa mwaka 1980 na nambari 2334 lililopitishwa mwaka 2016. Ukiukaji huo wa wazi wa sheria na maazimio ya kimataifa unaofanywa na Marekani unakusidia kufikia malengo mawili muhimu. Lengo la kwanza ni kubadili uwiano wa kieneo Mashariki ya Kati baada ya kushindwa njama za kuligawa eneo hili katika maeneo yanayotii amri na kudhamini maslahi ya Marekani, njama ambazo kwa haki zilifeli kufuatia kushindwa magaidi wa Daesh katika eneo na vilevile kukwamba siasa za hujuma za Saudi Arabia huko Yemen. Lengo la pili ni kudhoofisha na kuziondoa harakati za mapambano ya Kiislamu nchini Lebanon na Palestina katika mkondo wa kukabiliana na uchokozi wa utawala haramu wa Israel na hivyo kuufanya utawala huo uishi katika mazingira ya utulivu kuhusiana na suala zima la Palestina.

Waislamu wa Tanzania wakiandama Siku ya Quds

Ukweli wa mambo ni kwamba Marekani ni mshirika wa moja kwa moja wa jinai za utawala wa kibaguzi wa Israel dhidi ya watu wa Palestina. Hivi sasa Marekani inatekeleza njama ambayo inalenga moja kwa moja moyo wa Plaestina na utambulisho wake halisi, yaani Quds Tukufu ili kusibakie tena nchi inayoitwa Palestina.

Kuhusiana na suala hilo Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi uadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa kulitetea taifa la Palestina na jukumu la watu wote na kusisitizia suala hilo kwa kusema: "Hatupasi kudhani kwamba mapambano dhidi ya utawala wa Kizayuni hayana faida yoyote, bali kwa idhini na uwezo wa Mwenyezi Mungu, mapambano hayo dhidi ya utawala huo wa Kizayuni yatakuwa na natija ya kuridhisha. Kama ambavyo harakati za mapambano ya Kiislamu zimepata mafanikio makubwa ikilinganishwa na miaka iliyopita."

Tags

Maoni