Mei 31, 2018 06:50 UTC
  • Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia: Lugha ya Vitisho Haitatui Matatizo ya Kimataifa

Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia Sergei Lavrov amesema masuala ya nyuklia ya Iran, Korea Kaskazini na mgogoro wa Ukraine ni masuala ambayo hayawezi kutatuliwa kwa lugha ya vitisho.

Lavrov aliyasema hayo Jumatano katika siku ya pili ya  kongamano la kila mwaka la kimataifa la Primakov Readings lililofanyika katika mji mkuu wa Russia, Moscow na kuongeza kuwa lugha ya vitisho na ubabe haiwezi kuwa na tija wala kutatua migogoro ya kimataifa.

Lavrov ameashiria sera ambazo zimekuwa zikifuatwa na Rais Donald Trump wa Marekani ambazo ni za ubabe na maamuzi ya upande mmoja na kusema kujiondoa katika mapatano ya nyuklia ya Iran maarufu kama  Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekeelzwaji, JCPOA,ni mfano wa wazi wa sera hizo.

Marekani imekuwa ikijiona kuwa ni polisi wa dunia na ina dhana potovu kuwa inapaswa kushughulikia masuala yote ya kimataifa tena kwa kutumia mabavu na nguvu za kijeshi na pia kupitia uwezo wake wa kiuchumi kwa kutegemea silaha ya vikwazo. Hivi sasa matukio katika uga wa kimataifa yanaashiria muelekeo wa uwepo wa ncha kadhaa za nguvu na hivyo sera za Marekani haziendani na uhalisia wa mambo duniani. Hivi sasa Marekani imechukua mkondo wa vitisho na utumiaji mabavu katika masuala kadhaa ya kimataifa.

Mnamo Mei 8, Trump alitangaza kwamba nchi yake imejiondoa katika JCPOA, mapatano ambayo yalikuwa baina ya Iran na nchi tano wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa pamoja na Ujerumani maarufu kama kundi la 5+1 pamoja na Umoja wa Ulaya.

Trump

Trump alitangaza kuwa  Marekani itaiwekea Iran vikwazo vya nyuklia ambavyo ilikuwa imevisimamisha kwa muda. Uamuzi huo wa Trump umepingwa vikali na nchi zingine zilizoafiki mapatano ya JCPOA. Federica Mogherini Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya alitoa taarifa punde baada ya tangazo la Trump na kusisitiza kuwa umoja huo utaendelea kushirikiana na Iran katika fremu ya mapatano ya JCPOA. Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, Russia na Chuna pia zilimpinga Trump na kutangaza bayana kuwa zitabakia katika mapatano ya JCPOA. 

Kuhusu mgogoro wa Ukraine, Marekani pia inaendeleza sera zake za vitisho dhidi ya Russia na hata kutekeleza vikwazo dhidi ya nchi hiyo.

Nikki Haley, Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa alitangaza hivi karibuni kuwa maadamu Russia hairejeshei Ukraine eneo la Rasi ya Crimea na haiondoi askari wake mashariki mwa Ukraine, Marekani haitafungamana na Mapatano ya Minsk na itaendelea kuiwekea nchi hiyo vikwazo."

Msimamo huu unaonyesha kuwa katika kufikia malengo yake, Marekani inategemea tu vitisho na  lugha ya mabavu. Wolfanga Kubicki, Naibu Spika wa Bunge la Ujeurmani amebainisha wasiwasi wake kuhusu sera za Marekani kuhusiana na jambo hilo.

Katika upande mwingine, tokea Trump aingie madarakani Marekani, amekuwa akitoa vitisho dhidi ya Korea Kaskazini na hata ametishia kutekeleza hujuma kwa kutumia silaha za nyuklia dhidi ya nchi hiyo. Hii ni katika hali ambayo madola mengine makubwa duniani kama vile Russia, China na hata Umoja wa Ulaya, yamekuwa yakisisitiza kuhusu kufanyika mazungnzo kwa lengo la kutatua mgogoro wa Rasi ya Korea. Madola hayo makubwa yamekuwa yakiikosoa Marekani kwa kutumia vitisho dhidi ya Korea Kaskazini.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa

Kwa ujumla tunaweza kusema kuwa, sera za maamuzi ya upande mmoja katika utawala wa  Trump zinaendelea kutokana na watawala wa Marekani kudhani kuwa bado nchi yao ndio dola pekee lenye nguvu duniani. Kwa msingi wa ndoto hiyo Marekani imekuwa ikitaka kuainisha hatima ya masuala yote muhimu duniani. Kwa mtazamo wa Russia, muelekeo huo wa Marekani unavuruga majukumu ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na hilo litapelekea kuenea hali ya utovu wa nidhani katika uga wa kimataifa.

Tags

Maoni