Jun 18, 2018 12:11 UTC
  • Kutenganishwa watoto na wazazi wao huko Marekani, kielelezo halisi cha ukiukaji wa haki za binadamu

Kufichuliwa habari ya sera za kutenganisha watoto wadogo na wazazi wao wahajiri katika mpaka wa Marekani na Mexico kumezusha wimbi kubwa la hasira na malalamiko makubwa ndani na nje ya Marekani dhidi ya siasa za Rais Donald Trump wa nchi hiyo.

Siasa zinazotekelezwa na serikali ya sasa zinazojulikana kama "ustahamilivu sifuri" dhidi ya wahajiri haramu zimedhihirisha ukandamizaji mkubwa wa moja kati ya haki za kimsingi za binadamu. Katika fremu ya siasa hizo, karibu watoto elfu mbili wa Mexico wametenganishwa na wazazi wao na kufungwa katika kambi tofauti zilizoko katika mpaka wa nchi hizo mbili. Maafisa wa serikali ya Marekani wanadai kuwa, wazazi wa watoto hao wamefanya uhalifu wa kuwatorosha watoto hao na kuwaingiza ndani ya Marekani; hivyo wanapaswa kutenganishwa nao. Hii ni pamoja na kuwa, kutenganisha watoto wachanga na wazazi wao kunatoa pigo kubwa la kiroho na kinafsi kwa watoto hao na kuwa sababu ya kusambaratika familia. Maafisa wenye misimamo ya kufurutu mipaka wa Marekani waliokusanyika katika serikali ya Donald Trump wanatarajia kuwa, wanaweza kukabiliana na suala la kijamii la wahajiri haramu kwa kutumia mbinu chafu na zisiyo za kibinadamu. Watu kama Waziri wa Sheria wa Marekani, Jeff Sessions wanaoshiriki kutekeleza siasa hizo wametumia hata kitabu cha Injili kwa ajili ya kuhalalisha kitendo cha kinyama cha kutenganisha watoto wachanga na wazazi wao, sawa kabisa na walivyofanya watetezi wa utumwa ambao walitumia Injili kuhalalisha biashara ya utumwa kwa kutumia kitabu hicho.

Pamoja na hayo siasa kali za kuwapiga vita wahajiri haramu na hata wahajiri halali wenye vitambusho vya kuishi Marekani, zimezusha malalamiko makubwa ndani ya Marekani kwenyewe. Imepangwa pia kwamba siku chache zijazo kutafanyika maandamano makubwa katika pembe mbalimbali za Marekani kupinga siasa za kinyama za kutenganisha watoto na wazazi wao wahajiri nchini Marekani. 

Waziri wa Usalama wa Ndani wa serikali ya Barack Obama, Jeh Johnson anasema: "Kutenganisha watoto wadogo na wazazi wao kwa shabaha ya eti kupambana na wahajiri haramu kunapingana na thamani za Kimarekani."   

Inatupasa kusema hapa kuwa, sera za kutenganisha watu kwa mujibu wa mbari au kaumu zao lina historia ya miaka mingi nchini Marekani. Yapata miaka 250 iliyopita watoto wa Wamarekani wenye asili ya Afrika katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo walikuwa wakitenganishwa na wazazi wao kabla na baada ya uhuru wa nchi hiyyo na kuuzwa kama bidhaa katika masoko ya watumwa. Katika kipindi hicho cha giza, watumwa hawakuwa hata na haki ya kulea watoto waliowazaa wao wenyewe! Baada ya kufutwa utumwa, siasa za kuwatenganisha watu kwa mujibu wa rangi na mbari zao pia ziliendelea kutekelezwa nchini humo na kutengeneza dunia mbili tofauti, yaani dunia yenye neema, hali bora na utajiri ya wazungu na watu weupe, na ile iliyojaa umaskini, njaa na mashaka ya watu weusi. 

Hivi sasa pia manzoni mwa muongo wa tatu wa karne ya 21 na katika kipindi cha sasa ambapo suala la kulindwa haki za binadamu linatambuliwa kuwa miongoni mwa haki za kimsingi za mwanadamu, maafisa a serikali ya Marekani wanatekelezsa na kutetea sera za kutenganisha watoto wachanga na wazazi wao sawa kabisa na zile zilizokuwa zikitekelezwa miaka 250 iliyopita nchini humo! Kwa sasa kunatumiwa vigezo vingine kwa ajili ya kuhalalisha siasa za kutenganisha watoto na wazazi wao ikiwa ni pamoja na uhajiri haramu. 

Wakati huo huo vyombo vya habari vya Marekani vimetoa ripoti za kutoweka watoto wa wahajiri haramu nchini humo. Kwa maneno mengine ni kuwa, mbali na mashaka makubwa ya kiroho na kinafsi yanayowapata wato na wazazi wao wanaotenganishwa kwa kosa eti la uhajiri haramu, vilevile kuna hatari ya kutoweka watoto hao au hata kuuzwa kwa magenge ya wahalifu na watendajinai nchini Marekani, suala ambalo linaweza kuwa fedheha kubwa kwa serikali inayopiga vita wageni na wahajiri ya Rais Donald Trump.         

Tags

Maoni