Jun 20, 2018 02:37 UTC
  • Azma ya Ulaya ya kutaka kujitenga na Marekani katika masuala ya kimataifa

Jean-Claude Juncker, Mkuu wa Kamisheni ya Ulaya hivi karibuni ametoa matamshi mapya kuhusu siasa za Marekani na kusema kuwa, dhana ya 'Marekani Kwanza' ya Trump imepelekea imeifanya nchi hiyo ibaki peke yake.

Akizungumzia mjadala wa kibiashara kati ya EU na Marekani, Claude Juncker ametaka kuchukuliwa msimamo wa kujiamini watu wa Ulaya na kusema: "Huu si mpambano wa papa kukabiliana na dagaa. Na ikiwa ni mpambano wa namna hiyo basi utakuwa ni baina ya papa mmoja kukabiliana na papa mwengine." Akizungumza na gazeti la Stuttgarter Nachrichten la nchini Ujerumani, Jean-Claude Juncker aliongeza kwa kusema:  "Vyovyote iwavyo Umoja wa Ulaya ni mwakilishi wa theluthi moja ya biashara ya dunia; na katika uga huu Trump hana mshirika. Katika uwanja huu Trump anatutazama sisi kwa jicho la dharau; lakini kikao cha karibuni cha G7 kimeonyesha kuwa mtazamo wa Trump wa 'Marekani Kwanza' umegeuka kuwa wa Marekani iliyobaki peke yake." 

Jean-Claude Juncker, Mkuu wa Kamisheni ya Ulaya 

Moja ya udhaifu wa Umoja wa Ulaya ni kuwa na siasa za pamoja za kigeni na kiusalama. Katika mkakati wa kuwa na muelekeo wa pamoja kiuchumi, EU imeweza kupiga hatua kubwa kiushirikiano baina ya nchi za Ulaya, lakini katika uga wa siasa za kigeni na sera za kiusalama umoja huo umekuwa ukikumbwa na tofauti nyingi kati ya wanachama wake. Moja ya mipasuko hiyo ni kuwa na muelekeo wa pamoja ndani ya mipaka ya eneo la Bahari ya Atlantiki mkabala na wa nje ya mipaka ya bahari hiyo. Uingereza ni mtetezi wa harakati ya kupanua wigo wa ushirikiano wa pamoja nje ya mipaka ya eneo la bahari ya Atlantiki ambapo katika hilo imekuwa ikijikurubisha sana katika mahusiano na Marekani sambamba na kubaki kwenye mwamvuli wa kisiasa na kiusalama na Ulaya. Mkabala wake ni Ufaransa ambayo inatetea dhana ya kuwa na Ulaya moja yenye taratibu zake yenyewe za kujitegemea kwa ajili ya kulinda usalama wake.

George Walker Bush, rais wa zamani wa Marekani

Kushindwa siasa za kupenda vita za George Walker Bush na kuingia madarakani Barack Obama aliyekuja na siasa za kuvutia ushirikiano wa pande kadhaa, kuliwezesha kwa kiasi kikubwa kuzikurubisha nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya na Marekani kwa upande wa siasa za kigeni na za kiusalama. Upeo wa juu wa ukuruba huo ulishuhudiwa katika mazungumzo ya nyuklia na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Mazungumzo ambayo yalikuja kukamilika kwa kufikiwa makubaliano yaliyojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji JCPOA. Ni makubaliano ambayo hadi sasa nchi za Ulaya zimekuwa na mtazamo wa pamoja juu ya namna ya kuamiliana na Iran na suala hilo linahesabika kuwa nukta muhimu katika umoja huo.

Barack Obama rais wa zamani wa Marekani ambaye naye alipanua mahusiano kati ya EU na US

Hata kama kuingia madarakani George Walker Bush mwaka 2000 nchini Marekani na kadhalika siasa za kujichukulia maamuzi ya upande mmoja za timu ya wahafidhina mamboleo waliokuweko Ikulu ya White House wakati huo kulisababisha mpasuko mkubwa katika Umoja wa Ulaya, lakini kuweko madarakani hivi sasa Donald Trump, ambaye ni mshupalia vita na vilevile mvutia maslahi ya nchi yake tu katika miamala ya kibiashara, kinyume na ilivyokuwa mwaka 2000, kumeziunganisha pamoja nchi za Umoja wa Ulaya na kuwa na mshikamano katika namna ya kukabiliana na sera za kujichukulia maamuzi ya upande mmoja za Washington. Hatua ya Trump ya kujiondoa katika makubaliano mengi ya kimataifa na kieneo na moja ya makubaliano muhimu zaidi kati ya hayo yakiwa ni yale ya nyuklia ya Iran JCPOA, imeonyesha kwamba washirika wa pande mbili za Atlantiki, wana tofauti za kimtazamo juu ya suala la tishio na usalama. Umoja wa Ulaya unaamini kwamba kulindwa mapatano ya nyuklia ya Iran ndiyo njia itakayodhamini usalama na mamlaka yake ya utawala. 

Trump yeye ameamua kuitenga nchi yake na Umoja wa Ulaya

Haya ndiyo kama aliyoyasema  Mamdouf, mwanadiplomasia wa zamani wa Latvia kupitia mtandao wa kijamii aliposema: "Wakati Rais Donald Trump na Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong-un walipokuwa wakisherehekea tangazo lao la vipengele vinne huko nchini Singapore, kuhusiana na 'kuiepusha Peninsula ya Korea na silaha za nyuklia', naye Federica Mogherini, Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya alikuwa wakati huo akihutubia bunge la umoja huo kuhusiana na madhara yatakayofuatia baada ya Marekani kujiondoa katika makubaliano ya nyuklia yenye ufanisi mkubwa." Hatua ya serikali ya Rais Donald Trump ya kuzipandishia ushuru baadhi ya bidhaa zinazoingia Marekani kutokea Ulaya tena bila ya kuzingatia maslahi ya mashirika ya EU pia yamezipa hakikisho nchi za Ulaya kuwa uhusiano wa waitifaki hao wa pande mbili za Atlantiki unakabiliwa na mpasuko wenye ufa mkubwa. Matamshi aliyotoa Jean-Claude Juncker, Mkuu wa Kamisheni ya Ulaya yanathibitisha ukweli huo.

Maoni