Jun 20, 2018 07:29 UTC
  • UN: Kulindwa JCPOA kuna umuhimu kwa usalama wa dunia

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema kulindwa makubaliano ya nyuklia ya Iran ni jambo lenye udharura mkubwa hususan katika kudhamini usalama wa dunia.

Antonio Guterres aliyasema hayo jana Jumanne mjini Oslo, katika mazungumzo yake na Ali Akbar Salehi, Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran (AEOI) na kuongeza kuwa, yeye binafsi yupo katika mazungumzo na pande nyingine zilizosalia kwenye makubaliano hayo yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji JCPOA, kwa ajili ya kuyanusuru.

Guterres ambaye alikutana na Salehi pambizoni mwa duru ya 16 ya mkutano wa Oslo Forum katika mji mkuu huo wa Norway, amesisitiza kuwa makubaliano hayo ya Vienna ya mwaka 2015 yana umuhimu mkubwa pia katika kulinda amani ya kimataifa na kuzifanikisha jitihada za kuzuia uzalishaji na uenezaji wa silaha za nyuklia duniani. 

Kwa upande wake, Ali Akbar Salehi, Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran (AEOI) amesema Iran haijafikia matarajio yake kuhusu matunda ya JCPOA, katika nyuga za uchumi, benki na uwekezaji huku akiutaka Umoja wa Ulaya kusimama dhidi ya uadui wa Trump.

Hatua ya upande mmoja ya Trump ya kuiondoa US kwenye JCPOA inaendelea kulaaniwa kote duniani

Itakumbukwa kuwa tarehe 8 Mei,  rais wa Marekani, Donald Trump alitangaza kuitoa nchi yake kwenye mapatano ya JCPOA licha ya kwamba Washington ilikuwa mstari wa mbele kuyafanikisha wakati wa urais wa Barack Obama.

Hata hivyo Federica Mogherini, Mkuu wa Siasa za Kigeni wa Umoja wa Ulaya alisema kuwa, kulindwa mapatano ya nyuklia ya JCPOA kuna umuhimu wa kiusalama kwa bara Ulaya na kwamba EU itaendelea kufungamana na mapatano hayo ya kimataifa.

Tags

Maoni