Jun 20, 2018 07:38 UTC
  • Kundi la Taliban laua askari 30 wa Afghanistan katika mkoa wa Badghis

Licha ya serikali ya Afghanistan kutangaza kurefusha muda wa usitishaji vita wa upande mmoja kwa siku 10 zaidi, kundi la wapiganaji wa Taliban ambalo limekataa pendekezo hilo limetekeleza mashambulizi makubwa mapema leo lilioua makumi ya askari wa nchi hiyo katika mkoa wa Badghis.

Gavana wa mkoa huo amesema wanajeshi 30 wa Afghanistan wameuawa na wengine kadha kujeruhiwa mapema leo baada ya wapiganaji wa Taliban kushambulia vituo viwili vya upekuzi, magharibi mwa mkoa huo.

Amesema hili ndilo shambulizi kubwa kuwahi kufanywa na genge hilo tangu baada ya kumalizika tangazo lake la usitishaji vita wa siku tatu uliomalizika Jumapili iliyopita.

Baada ya kutangaza usitishaji mapigano kwa muda wa siku tatu kwa mnasaba wa Sikukuu ya Idul-Fitr, wapiganaji wa kundi la Taliban alfajiri ya kuamkia juzi walianzisha tena mashambulio dhidi ya ngome za vikosi vya usalama vya serikali ya Afghanistan.

Rais Ashraf Ghani wa Afghanistan

Itakumbukwa kuwa, Juni 12, serikali ya Rais Ashraf Ghani ilitangaza usitishaji vita wa upande mmoja wa kuendelea kwa muda wa siku tano baada ya Idul-Fitri. Kufuatia hatua hiyo, kundi la Taliban, nalo pia lilitangaza usitishaji mapigano kwa muda wa siku tatu za maadhimisho ya Sikukuu hiyo tukufu.

Mapema mwezi uliopita, Rais Ghani alitangaza kwa mara ya kwanza kuwa Taliban inapasa itambuliwe kama kundi la kisiasa lililo halali na la kisheria, mkabala wa kundi hilo kuitambua rasmi serikali ya Afghanistan.

Tags

Maoni