Jun 23, 2018 02:22 UTC
  • Radiamali ya China na Australia kuhusu kujitoa Marekani katika Baraza la Haki za Binadamu

China na Australia zimesikitishwa sana na hatua ya Marekani kujitoa katika Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa.

Akizungumza hivi karibuni na waandishi wa habari, Geng Shuang, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China amesema kuwa ni jambo la kusikitisha mno kwa Marekani kujitoa katika baraza hilo la haki za binadamu kwa kuzingatia shughuli zake muhimu za kusimamia haki za binadamu duniani. Waziri wa Mambo ya Nje wa Asutralia pia amesikitishwa sana na hatua hiyo isiyo ya kimantiki ya Marekani. Awali Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na wakuu wa shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch pia walikuwa wameelezea kusikitishwa na hatua hiyo ya  Marekani. Siku ya Jumanne, Mike Pompeo na Nikki Haley, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani na mwakilishi wa nchi hiyo katika Umoja wa Mataifa kwa utaratibu huo, walitangaza kujiondoa nchi hiyo katika Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa. Baraza hilo ambalo lina wanachama 47 lina nafasi muhimu katika kuimarisha na kulinda haki za binadamu katika pembe tofauti za dunia.

Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa

Hatua hiyo ya Marekani inatathminiwa kuwa mwendelezo wa siasa zake za upande mmoja katika ngazi za kimataifa. Siasa hizo zilianza kutekelezwa wakati wa utawala wa rais wa zamani wa Marekani, George W. Bush, kufuiatia mashambulio ya kigaidi ya 2001. Siasa hizo za kibabe zimepata msukumo mpya katika utawala wa Rais Donald Trump ambaye amekuwa akipuuza na kukanyaga waziwazi mapatano na mikataba yote muhimu ya kimataifa kwa kisingizio cha kudhamini maslahi ya taifa la Marekani chini ya nara potovu ya 'Marekani Kwanza.' Kujitoa Marekani katika mikataba muhimu ya kimataifa kama vile mapatano ya nyuklia ya Iran na nchi sita muhimu za dunia mashuhuri kama JCPOA, mkataba wa kibiashara wa Trans-Pacific na mkataba wa tabianchi wa Paris ni baadhi ya mikataba muhimu ambayo Marekani imeipuuzilia mbali tokea kuingia madarakani Trump. Hatua ya Marekani kuendelea kupuuza na kujitoa katika mikataba na taasisi muhimu za kimataifa na hasa hatua yake ya hivi karibuni ya kujitoa katika Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa imekemewa na kukosolewa vikali katika ngazi za kimataifa. Uamuzi wa Marekani kujiondoa katika Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa na ambao umechukuliwa kufuatia kukosolewa na baraza hilo jinai zinazotekelezwa na utawala ghasibu wa Israel dhidi ya Wapalestina wasio na hatia, ni jambo linaloonyesha wazi kwamba White House inashirikiana kwa karibu na utawala huo katili na haramu katika kudumisha mauaji ya kutisha dhidi ya Wapalestina.

Mkataba wa tabianchi wa Paris

Licha ya kuwa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa ni uwanja wa kujadiliwa na kuchunguzwa njia za kulindwa haki za binadamu katika maeneo tofauti ya dunia, lakini baraza hilo hadi sasa halijachukua hatua yoyote kujadili ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu za jamii za wachache na hasa jamii ya watu weusi nchini Marekani kutokana na mashinikizo ya White House dhidi ya kujadiliwa suala hilo katika baraza hilo. Ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu unaoendelea nchini Marekani dhidi ya jamii hizo za wachache hata ulimpelekea Barack Obama rais wa zamani wa nchi hiyo kukiri kwamba bado kuna mfumo wa utumwa nchini humo. Msimamo huo wa Obama ulichukuliwa kufuatia kuuawa raia 9 weusi wa nchi hiyo na Mmarekani mweupe mmbaguzi wa rangi katika Kanisa la Charleston mwaka 2016. Kufuatia tukio hilo la kutisha la ubaguzi wa rangi, Obama alikiri kwamba mfumo wa utumwa na ukiukwaji wa haki za kiraia ungali hai huko Marekani.

Mabomu ya nyuklia yaliyotumiwa na Marekani kuangamiza wakazi wa Nagasaki na Hiroshima, Japan

Ukiukwaji huo wa haki za binadamu dhidi ya watu weusi unaendelea kushuhudiwa nchini Marekani katika hali ambayo nchi hiyo imekuwa ikitumia kisingizio cha haki hizo kama chombo cha kutoa mashinikizo dhidi ya nchi nyingine huru na zinazojitawala ambazo zinapinga siasa za ubabe za nchi hiyo katika ngazi za kieneo na kimataifa. Kuhusu hilo Manlio Dinucci, mwandishi wa Italia anasema kuwa Marekani ni nchi ya kwanza kuwahi kukiuka hazi za binadamu duniani kwa kutumia silaha za nyuklia dhidi ya watu wa miji ya Hiroshima na Nagasaki nchini Japan.

Radiamali hasi ya Australia kuhusiana na hatua ya hivi karibuni ya Marekani kujitoa katika Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa, nchi ambayo inahesabiwa kuwa mshirika wa kieneo wa Marekani, inathibitisha wazi kwamba hata washirika wa karibu wa Marekani hawaridhishwi na hatua za upande mmoja zinazochukuliwa na nchi hiyo katika upeo wa kimataifa.

Maoni