Jun 23, 2018 06:59 UTC
  • Mahakama ya ICC yaipa muhula wa mwisho serikali ya Myanmar

Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) Imetoa taarifa ikiipa muhula wa mwisho serikali ya Myanmar kujibu tuhuma zinazohusiana na jinai kubwa zinazofanywa nchini humo dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya.

Taarifa hiyo ya mahakama ya ICC imeainisha tarehe 27 Julai mwaka huu wa 2018 kuwa muda wa mwisho kwa serikali ya Myanmar kufika mbele ya majaji wa mahakama hiyo mjini The Hague ili kujibu tuhuma zinazohusiana na mauaji na uhalifu mkubwa unaofanyika nchini humo dhidi ya Waislamu wa Rohingya.

Mwendesha Mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, Fatou Bensouda, yapata miezi mitatu iliyopita aliwataka majaji wa mahakama hiyo kutoa kibali cha kufanyika uchunguzi juu ya operesheni za kuhamishwa na kufukuzwa kwa mabavu zaidi ya Waislamu laki nane wa jamii ya Rohingwa huko Myanmar. Watu hao wamekimbilia nchini Bangladesh. 

Image Caption

Kabla ya hapo mamia ya raia wa jamii ya Rohingya ambao watu wa familia zao waliuawa katika ukatili wa Mabudha wa Myanmar au wao wenyewe wamekuwa wahanga wa ukatili huo kwa njia moja au nyingine walikuwa wameiomba Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kumruhusu mwendesha mashtaka wake kuchunguza mauaji na vitendo ya kuwafukuza maelfu ya Waislamu na kuwalazimisha kukimbilia nje ya nchi. 

Uamuzi wa sasa wa mahakama hiyo wa kuitaka serikali ya Myanmar kufika mbele ya mahakama hiyo hadi kufikia tarehe 27 Julai ni hatua mpya ya kufuatilia jinai na uhalifu uliopelekea kuuawa maelfu ya raia wasio na hatia na kuwalazimisha wengine karibu milioni moja kukimbilia Bangladesh. Japokuwa inasemekana kwamba, itakuwa vigumu kwa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai kushughulikia jinai zilizofanywa na jeshi la Myanmar dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya nchini humo kutokana na ukweli kwamba, Myanmar si mwanachama wa mahakama hiyo, lakini inasemwa kuwa mahakama ya ICC imeingia katika faili hilo kupitia njia ya Bangladesh ambayo ni nchi mwanachama.

ICC inapaswa kushughulikia mauaji ya Waislamu wa Rohingya, Myanmar

Kwa mujibu wa hati ya Mahakama ya ICC, majaji wa mahakama hiyo wanapaswa kushughulikia jinai za kivita, jinai dhidi ya binadamu, mauaji ya kimbari na uhalifu kama wa ubakaji vilivyofanywa na Mabudha wa Myanmar wakisaidiwa na jeshi la nchi hiyo dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya. Vilevile wanapaswa kusitisha mauaji ya kimbari na jinai dhidi ya binadamu vinavyoendelea kufanyika nchini humo na kuwapandisha kizimbani watenda jinai hizo.

Maelfu ya Waislamu wa Rohingya wameuawa Myanmar

Antoine Cartalochi ambaye ni mtaalamu wa jiografia ya kisiasa anasema: Yanayotokea katika mkoa wa Rakhine nchini Myanmar ni mauaji ya kimbari dhidi ya jamii ya waliowachache ya Rohingya. Japokuwa  Mahakama ya Kimataifa ya Jinai imechukua hatua ya kushughulikia jinai na uhalifu huo ulioanza Agosti mwaka 2017 kwa kuchelewa, lakini walimwengu wanatarajia kuwa, taasisi hiyo itawachukulia hatua stahiki watenda jinai na mauaji hayo ya kutisha na kutayarisha mazingira mazuri ya kurejea nyumbani maelfu ya wakimbizi wa Rohingya."        

Maoni