Jul 11, 2018 07:43 UTC
  • Polisi India watakiwa kupunguza uzito na vitambi, vinginevyo watafukuzwa kazi

Idara ya polisi nchini India imewaamuru maafisa wake kupunguza uzito wa mwili vinginevyo watasimamishwa kazi.

Mkuu wa idara hiyo katika jimbo la Karnataka amewaambia waandishi wa habari kwamba, ana wasiwasi mkubwa kutokana na kuongezeka idadi ya maafisa wa polisi wenye vitambi.

Bhaskar Rao amesema kuuwa, amechukua uamuzi huo baada ya maafisa zaidi ya 100 kupoteza maisha katika kipindi cha miezi 18 pekee iliyopita kutokana na maradhi yaliyo na uhusiano wa moja kwa moja na mtindo wa maisha

Ripoti zaidi kutoka nchini India zinasema kuwa, maafisa wa polisi wenye uzito wa ziada na vitambi watapatiwa ushauri na usaidizi kwa ajili ya kubadili mfumo wa maisha na namna ya kula.

Bhaskar Rao, Mkuu wa Idara ya Polisi katika jimbo la Karnataka

Idara ya Polisi katika jimbo hilo lina askari 14,000, ambao husimamia usalama wakati wa matukio makubwa na kudhibiti maandamano na vurugu.

Tayari kumetolewa amri ya kuwatambua maafisa wenye uzito mkubwa na kuwaweka katika mpango wa kufanya mazoezi ili kupunguza uzito.

''Tumeanza kazi ya kuwafuatilia maafisa kwa kupima sukari na vipimo vingine miezi sita iliyopita. Hatua hii mpya ya kusimamishwa kazi ni kitisho kwa wale wasiojali afya zao'', amesema Mkuu wa Idara ya Polisi katika jimbo la Karnataka.

Inaelezwa kuwa, takribani polisi 150 hupoteza maisha kila mwaka nchini India kutokana na maradhi yaliyo na uhusiano wa moja kwa moja na mtindo wa maisha (lifestyle).

Maoni