Jul 11, 2018 13:21 UTC
  • Marekani yalegeza msimamo wa vikwazo dhidi ya Iran baada ya kuonywa

Marekani imelegeza msimamo wake mkali wa kuiwekea Iran vikwazo na kuzuia mafuta ghafi ya petroli ya nchi hii kuuzwa katika soko la kimataifa ifikapo Novemba 4.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mike Pompeo ametangaza kuwa Washington imeamua kuziruhusu nchi zinazotaka kununua mafuta ya Iran zifanye hivyo. Tangazo hilo linaashiria kuwa Marekani imelegeza msimamo wake mkali wa awali ambapo Rais Donald Trump wa Marekani alikuwa ameapa kuhakikisha kuwa uuzaji mafuta ghafi ya petroli ya Iran utafikia sufuri mwezi Novemba.

Akizungumza mjini Abu Dhabi katika mahojiano na Televisheni ya Sky News Arabia, Pompeo amesema kuna nchi kadhaa ambazo zimeitaka Marekani isizizuie kununua mafuta ya Iran. Marekani imetahadharishwa kuwa jaribio lolote la kuzuia mafuta ya Iran yafike katika soko la kimataifa ni jambo ambalo litapelekea bei ya mafuta ya petroli kuongezeka zaidi ya mara tatu ya hivi sasa.

Kati ya nchi ambazo zimetangaza kuiomba Marekani iziruhusu kununua mafuta ya Iran ni Japan na Korea Kusini nazo nchi kama vile China, India na Uturuki zimesema zitapuuza kikamilifu vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran.

Mstari wa rangi nyekundu unaonyesha Lango Bahari la Hormuz

Nchi kadhaa za Ulaya nazo pia zinatazamiwa kuifahamisha Marekani kuwa zitanunua mafuta ya Iran na hivyo haziafiki nchi hii kuwekewa vikwazo.

Akiwa Uswizi wiki iliyopita, Rais Hassan Rouhani wa Iran alitahadahrisha kuwa Iran haitaruhusu mafuta ya nchi jirani yasafirishwe katika soko la kimataifa iwapo  itazuiwa kuuza mafuta yake. Rais Rouhani alikuwa akiashiria kwa njia isiyo ya moja kwa moja kuwa Iran inaweza kufunga Lango Bahari la Hormuz ambalo ni njia ya kusafirishia asilimia 35 ya mafuta yote duniani.

 

Tags

Maoni