Jul 12, 2018 07:15 UTC
  • Mwaka wa 23 wa kumbukumbu ya mauaji ya Srebrenica; nembo nyingine ya fedheha ya haki za binadamu za Magharibi

Katika kumbukumbu ya mwaka wa 23 wa mauaji ya Waislamu wa Bosnia katika mji wa Srebrenica zaidi ya watu 6,000 wameshiriki katika matembezi ya 'Mars Mira' na kufika katika kijiji cha Potocari ambacho ndicho kituo cha kumbukumbu ya wahanga wa mauaji hayo ya halaiki.

Mars Mira au "Matembezi ya Amani" ni sehemu ya kumbukumbu ya mauaji ya Waislamu wa Bosnia ambayo hufanywa kila mwaka kuwakumbuka wahanga wa maafa hayo ya kibinadamu. Tarehe 11 Julai 1995, Waislamu wapatao 10,000 waliomba hifadhi katika kambi ya Umoja wa Mataifa katika mji wa Srebrenica kwa hofu ya kuuawa na jeshi la Serbia.

Eneo hilo lililokuwa limeanzishwa na askari wa Uholanzi na kutajwa na Umoja wa Mataifa kama eneo salama. Askari wa Uholanzi ambao walikuwa na jukumu la kulinda amani katika eneo hilo, siku hiyo hiyo wakalikabidhi eneo hilo kwa wanamgambo wa Kiserbia. 

Majeshi ya Serbia yakiongozwa na Jenerali Ratko Mladic yaliwateka nyara wanaume na vijana wapatao 8,500 wa Srebrenica. Kwa mujibu wa asasi za kimataifa Waislamu hao waliuawa kwa umati hadi Julai 19 na maiti zao kukusanywa kwa mabuldoza na malori na kuzikwa katika makaburi kadhaa ya umati katika maeneo ya msitu katika viunga vya mji huo.

Jenerali Ratko Mladic, mmoja wa watuhumiwa wakuu wa mauaji ya Waislamu wa Bosnia 1995

Hadi sasa miili 6,575 ya wahanga wa mauaji ya halaiki ya Srebrenica imepatikana na kuzikwa na juhudi za kuipata miili mingine zingali zinaendelea. Mauaji hayo ya umati yanahesabiwa kuwa makubwa zaidi kuwahi kutokea barani Ulaya baada ya Vita vya Pili vya Dunia

Mtuhumiwa mkuu wa mauaji hayo alikuwa Jenerali Ratko Mladic kamanda wa zamani wa jeshi na Radovan Karadžić Rais wa zamani wa Srpska na majimui ya makamanda wa jeshi la Srpska. Serikali ya Uholanzi inasisitiza kwamba, wahusika wa mauaji hayo ni Waserbia wa Bosnia  na sio vikosi vya nchi hiyo. Mwanaume mmoja Mwislamu ambaye alinusurika mauaji hayo anasema: Ninazitafadhalisha nchi zote za dunia ziyatambue mauaji haya ya halaiki. Tuyatambue mauaji haya bila kuzingatia ni nchi gani au taifa gani lilisababisha kutokea mauaji haya na wahanga walikuwa akina nani, ili katika historia yasije kukaririwa tena mauaji kama haya.

 

Kofi Annan, alikuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wakati mauaji ya Srebrenica yalipotokea

Umuhimu wa suala la mauaji ya Srebrenica unatokana na kuwa, mauaji hayo yalitokea mbele ya macho ya vikosi vya Uholanzi vilivyokuwa sehemu ya kikosi cha kusimamia amani cha Umoja wa Mataifa  na yalitokea katika eneo ambalo lilitangazwa na Umoja wa Mataifa kuwa ni eneo salama na vilevile Umoja wa Mataifa ulikuwa umechukua jukumu la kulinda eneo la Srebrenica kwa mujibu wa maazimio yaliyokuwa yamepasishwa na Baraza la Usalama. 

Kwa hakika jinai hiyo ya kihistoria inaweza kutajwa moja kwa moja kuwa ni natija ya hatua za kigugumizi za vikosi vya kusimamia amani vya Umoja wa Mataifa mkabala na Waserbia na ni kutotekeleza majukumu yake ya kuwalinda watu wa Srebrenica

Kumbukumbu ya wahanga wa mauaji ya Srebrenica

Jinai hiyo ilikuwa kubwa mno kiasi kwamba, Kofi Annan Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wakati huo alisema kuwa, Srebrenica daima itaendelea kuitesa na kuiadhibu nafsi na dhamira ya umoja huo na akasema kuwa, haya ni mafaa makubwa kabisa ya kivita kuwahi kutokea baada Vita vya Pili vya Dunia. Mark Brown, mjumbe maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mtaifa wakati huo naye anayatambua mauaji ya umati ya Waislamu wa Bosnia huko Srebrenica kuwa, ni jambo ambalo daima litaendelea kutia doa historia ya umoja huo.

Pamoja na hayo, swali la kimsingi linaloulizwa ni hili kwamba, je, Umoja wa Ulaya na Shirika la Kijeshi la NATO hazikuyaona mauaji hayo hata zitoe radiamali kuhusiana nayo? Na je, vikosi vya Uholanzi havikuwa na jukumu lolote lile la kulinda roho za raia hao wengi na ambao hawakuwa na hatia hata ikafikia kwamba, vikosi hivyo vikawa tayari kuwatoa wahanga wananchi hao na vyenyewe kusalimisha roho na uhai wao?

Tags

Maoni