Jul 12, 2018 09:33 UTC
  • Trump aibua mifarakano katika muungano wa kijeshi wa NATO

Siku ya kwanza ya kikao cha viongozi wa muungano wa kijeshi wa nchi za Magharibi, NATO, imemalizika huku mkutano huo ukishuhudia mashambulizi makali ya maneno ambayo hayajawahi kushuhudiwa ya Rais Donald Trump wa Marekani dhidi ya Ujerumani, moja kati ya nchi muhimu zaidi katika muungano huo wa NATO.

Kama ilivyotarajiwa, kikao cha NATO katika mji mkuu wa Ubelgiji, Brussels kimebadilika na kuwa medani ya majibizano makali baina ya Trump na Kansela Angela Merkel wa Ujerumani.

Mapema Jumatano baada ya mkutano wake na Jens Stoltenberg Katibu Mkuu wa Muungano wa Kijeshi wa NATO, Trump aliitaja Ujerumani kuwa  ni nchi iliyotekwa na Russia. Trump aliongeza kuwa: "Sisi katika NATO tuntoa gharama kubwa kwa ajili ya usalama wa Ujerumani , Ufaransa na nchi zingine nyingi ili ziweze kukabiliana na tishio tarajiwa la Russia. Lakini pamoja na hayo, hao waitifaki wetu wanatia saini mapatano muhimu zaidi na Russia. Asilimia  70 ya mahitajio ya nishati ya Ujerumani yanakidhiwa na Russia.

Matamshi ya Trump yalikuwa kinaya ya wazi kwa nchi za Magharibi na hasa Ujerumani ambayo pamoja na kuwepo mikakati maalumu ya NATO ya kukabiliana na kile kinachodaiwa ni tishio kutoka Russia, inaendelea kuwa na uhusiano mzuri na wa karibu na Moscow hasa katika uga wa nishati. Kuhusiana na hilo hivi sasa Ujerumani inashirikiana na Russia katika ujenzi wa bomba la gesi linalojulikana kama Nord Stream 2 ambalo litasafirisha gesi ya Russia hadi Ujerumani kupitia Bahari ya Baltiki. Mradi huo unakadiriwa kugharimu Euro bilioni 9.5. Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, kama ilivyotarajiwa, amejibu matamshi makali ya Trump kwa kusema: "Ujerumani iko huru katika kuchagua na kutekeleza sera zake."

Bendera ya NATO

Wakuu wengine wa Ujerumani nao pia wamejibu matamshi hayo ya kiburi ya Trump. Heiko Maas Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani katika kujibu matamshi ya Trump amesema: Ujerumani si mateka wa Russia bali ni mdhamini wa uhuru duniani.

Suala jingine muhimu hapa ni kuwa, hitilafu zinazoongezeka baina ya Marekani na Ujerumani zimebadilika na kuwa suala lenya kuzisababishia hasara ya kijeshi nchi nyingine wanachama wa NATO. Mwaka 2014 wanachama wa NATO walikubaliana kuwa ifikapo mwaka 2024 kila nchi itakuwa inatumia asilimia mbili ya pato ghafi la taifa kwa ajili ya bajeti ya muungano huo wa kijeshi. Trump anadai kuwa ni nchi 8 tu kati ya 29 za muungano huo ndizo zimezingatia kigezo hicho.

Njia ya Bomba la Gesi kutoka Russia hadi Ujerumani

Wakati huo huo Trump, kabla ya kikao cha wiki hii cha NATO alikuwa amezitaka nchi wanachama zitumie hadi asilimia 4 ya pato ghafi la ndani kwa ajili ya bajeti ya kijeshi huku akidai kuwa asilimia mbili iliyokuwa imetangazwa hapo awali haitoshi. Trump ameashiria fedha ambazo Ujerumani inatumia kugharamia ujenzi wa bomba la gesi kutoka Russia na  kusema nchi wanachama wa NATO zinapaswa kuanza kuongeza bajeti ya shirika hilo la kijeshi hivi sasa na zisisubiri mwaka 2025. Mamtamshi hayo ya Trump yamekosolewa vikali na Ujerumani.

Katika kukosoa matamshi ya Trump anayedai kuwa Mrekani ndiyo inayoongoza katika utoaji wa bajeti kwa NATO, Kansela Merkel wa Ujerumani amesema: "Ujerumani pia imefanya kazi kubwa ndani ya NATO. Ujerumani ni nchi ya pili inayochangia askari katika jeshi la NATO na hivi sasa inashiriki pakubwa katika oparesheni ya NATO nchini Afghanistan." Merkel amesema kuwa nchi yake pia inatetea maslahi ya Marekani.

Msimamo huo uliotangazwa na Merkel pia umeungwa mkono na Donald Tusk Mkuu wa Baraza la Ulaya ambaye amesema nchi za Ulaya zimekuwa na mchango mkubwa katika bajeti ya NATO. Amesema nchi za Ulaya zina bajeti kubwa ya kijeshi kuliko nchi kama vile China na zimekuwa zikishiriki katika kukidhi bajeti ya NATO.

Tags

Maoni