Jul 12, 2018 14:57 UTC
  • Erik Prince: Trump anakusudia kubinafsisha vita vya Afghanistan

Mkuu wa zamani wa shirika la usalama la Blackwater lenye mafungamano na Marekani na utawala wa Kizayuni, ameelezea azma ya Washington ya kubinafsisha vita vya Afghanistan.

Erik Prince ameyasema hayo katika mahojiano na gazeti la Uingereza la The Independent kuhusiana na takwa la Rais Donald Trump wa Marekani la kuongeza idadi ya askari wa kigeni nchini Afghanistan katika fremu ya muungano wa kijeshi wa nchi za Magharibi, NATO na kusema kuwa, kile ambacho Trump anatakiwa kukisema kwa muungano huo ni kwamba, kutumwa askari zaidi kwenda nchi hiyo ya Asia ya Kati hakuna faida, na badala yake wanachama wa NATO wanatakiwa kutuma fedha zaidi.

Prince ameongeza kwamba, serikali ya Marekani kwa mwaka inatumia kiasi cha Dola bilioni 76 nchini Afghanistan na inaamini kwamba, mpango wa kuwakabidhi askari wa mashirika ya usalama ya Marekani jukumu la vita vya Afghanistan, utapunguza gharama za vita hivyo.

Erik Prince, Mkuu wa zamani wa Shirika la Usalama lenye mafungamano na Marekani na utawala wa Kizayuni, Blackwater

Inafaa kuashiria kuwa, mwaka 2012, serikali ya Kabul, mji mkuu wa Fghanistan ilitangaza kwamba harakati za mashirika ya usalama ya kigeni nchini humo ni kinyume cha sheria na badala yake jukumu la usalama wa nchi liko mikononi mwa polisi ya nchi hiyo. Kufuatia tangazo hilo, mamia ya mashirika ya kigeni yaliyokuwa yanajihusisha na masuala ya usalama nchini Afghanistan yalitimuliwa, isipokuwa mashirika makubwa ya usalama na yanayoungwa mkono na Wizara ya Ulinzi ya Marekani, Pentagon na mashirika ya upelelezi ya nchi hiyo ndio yaliendeleza shughuli zake. 

Shirika la Blackwater ambalo ni moja ya makampuni makubwa ya kandarasi ya shirika la ujasusi la Marekani CIA, na ambalo linatuhumiwa mara kwa mara kuhusiana na kufanya ukatili na utesaji dhidi ya raia, bado linaendesha shughuli zake nchini Afghanistan.

Tags

Maoni