• Trump: Vikwazo vya Russia havitaondolewa na hakuna muhula kuhusu mazungumzo na Pyongyang

Rais wa Marekani amesema katika mazungumzo na wabunge wa nchi hiyo huko White House kuwa hakuna uwezekano wa kufutwa vikwazo dhidi ya Moscow na kwamba vikwazo hivyo vitaendelea kuwepo licha ya kufanyika mazungumzo na Rais Vladimir Putin wa Russia.

Trump amedai kuwa Putin ameafiki maoni yake kuhusu Korea ya Kaskazini na kueleza kuwa Russia imemuhakikishia kuwa itaunga mkono mazungumzo ya kuipokonya silaha Korea ya Kaskazini na akasisitiza kuwa hakuna muhula wowote ulioainishwa kwa ajili ya mazungumzo hayo. Matamshi hayo ya Trump yanatolewa katika hali ambayo huko nyuma alisisitiza kuwa suala la kuipokonya silaha Korea ya Kaskazini linapasa kufanyika haraka. Ulegezaji msimamo huo wa mara kwa mara wa Trump unaonyesha namna rais huyo wa Marekani asivyo na misimamo imara. Kwa kutoa matamshi kama haya, Rais wa Marekani amedhihirisha namna anavyoweza haraka kulegeza na kubadili misimamo yake akiwa chini ya mashinikizo. 

Marais wa Marekani na Russia katika mkutano na waandishi wa habari mjini Helsinki, Finland

Hii ni mara ya pili ambapo Rais wa Marekani anaonekana kulegeza misimamo na matamshi yake  katika muda wa siku chache zilizopita. Wakati vombo vya habari, fikra za waliowengi na wasomi nchini Marekani walipoushambulia mkutano kati ya Rais wa Marekani na mwenzake wa Russia Vladimir Putin na waandishi wa habari na uungaji mkono wa Trump kwa Moscow, Rais huyo wa Marekani alilazimika  kurekebisha matamshi yake hayo siku moja tu baada ya mkutano huo na badala yake kutangaza kuwa anaunga mkono kikamilifu uchunguzi wa idara za kiitelijinsia za Marekani. Kutoaminiwa Rais wa Marekani kumefikia kiwango ambacho wawakilishi wa kongresi ya nchi hiyo wanataka kuwaita na kuwahoji  wakalimani wa  mazungumzo ya siri ya marais hao wawili; na kwa njia hiyo ili kuweza kujiridhisha kwanza na kile kilichozungumzwa iwapo Rais Trump hakuyatumbukiza hatarini maslahi ya kitaifa ya nchi yao. Hotuba aliyoitoa  Trump katika kikao huko Helsinki pamoja na Rais Vladimir Putin hadi sasa haijaidhinishwa na ikulu ya Russia, Kremlin; na hatua hiyo ya Moscow imezidisha shaka kuhusu usahihi wa hotuba hiyo ya Rais wa Marekani. 

Aidha matamshi na misimamo hiyo ya Trump kuhusu Iran na Korea ya Kaskazini yamekuwa na mkondo usioweza kuaminika na yamekoselewa vikali na wasomi wa kisiasa wa Marekani na ulimwenguni kwa ujumla. Wakati huo huo radiamali iliyotolewa na viongozi wa kisiasa na vyombo vya habari nchini Marekani kwa matamshi hayo ya Trump na Putin inaonyesha kuwa kikao hicho hakiwezi kuwa na taathira kubwa kwa uhusiano wa pande mbili. Kwani huko Washington Trump anachukuliwa kuwa mshindwa wa mazungumzo hayo. 

Sergey Karaganov mchambuzi mtajika na Mkuu wa Baraza la Sera za Ulinzi na Kigeni la Russia anasema: Si jambo lililo mbali kuzidi kuwa mbaya hali ya mambo katika uhusiano kati ya Russia na Marekani kwa sababu huenda watu wa karibu na Trump wakamchochea kuchukua hatua dhidi ya Russia kutokana na shakhisia isiyotabirika ya rais huyo wa Marekani.   

Tags

Jul 19, 2018 08:20 UTC
Maoni