• Mbunge wa chama tawala Marekani ataka Trump auzuliwe

Mbunge wa chama tawala cha Republican nchini Marekani amekosoa vikali utendaji wa Rais Donald Trump wa nchi hiyo na kutoa wito wa kusailiwa na kupigiwa kura ya kutokuwa na imani naye katika Kongresi ya nchi hiyo.

Jason Villalba ambaye ni mbunge wa chama cha Republican kwa tiketi ya jimbo la Texas amesema kuwa, tangu Donald Trump aliposhika madaraka ya nchi, deni la taifa la Marekani limeongezeka na kufikia dola zaidi ya trilioni moja na kwamba deni la taifa halijawahi kuongezeka kwa kasi hiyo katika kipindi cha rais yeyote wa Marekani katika kipindi chote cha historia. 

Villalba ameongeza kuwa, Trump amekebehi na kuchezea shere sheria za uhamiaji, taasisi na mashirika ya ujasusi, siasa za nje na hata wananchi wa Marekani.

Mbunge huyo wa chama cha Republican amewataka wapiga kura wa Marekani wasimpe kura zao kiongozi huyo katika uchaguzi ujao. Amesema Trump si rais wa Marekani tena na sasa umewadia wakati wa kumtupa katika fuko la taka la historia kwa kumpigia kura ya kutokuwa na imani naye. 

Donald Trump

Wito wa mbunge huyo wa Texas umetolewa baada ya wabunge wa vyama vyote viwili vikubwa vya Marekani kukosoa vikali utendaji wa Rais Donald Trump katika mkutano wake na waandishi wa habari akiwa pamoja na Rais Vladimir Putin wa Russia mjini Helsinki Jumatatu iliyopita. 

Alipoulizwa kuhusu madai kwamba Russia iliingilia uchaguzi wa Rais nchini Marekani katika mkutano huo Trump alijibu kwamba: Hakuna ushahidi wowote unaothibitisha kwamba Russia iliingilia uchaguzi huo. Matamshi hayo ni kinyume na ripoti zilizotolewa na taasisi za upelelezi za Marekani zinazodai Russia iliingilia zoezi la Uchaguzi wa rais uliomfikisha madarakani Donald Trump dhidi ya mpinzani wake, Hillary Clinton.   

Tags

Jul 19, 2018 15:35 UTC
Maoni