• Safari ya rais wa china katika nchi tano za Kiarabu na Kiafrika

Siku ya Alkhamisi Rais Xi Jinping wa China alianza safari ya siku kumi ya kizitembela nchi tano za Kiarabu na Kiafrika.

Katika safari yake ya nchi za Imarati, Senegal, Rwanda, Afrika Kusini na Mauritius Rais Xi Jinping ataonana na kuzungumza na wakuu wa nchi hizo kuhusiana na masuala mbalimbali ya kuimarisha uhusiano wa pande mbili. Akiwa Afrika kusini kati ya tarehe 25 hadi 27 Rais  Jinping anatazamiwa kushiriki katika kikao cha wakuu wa nchi wanachama wa jumuiya ya kibiashatra ya BRICS kinachotazamiwa kufanyika mjini Johannesburg. Jumuiya hiyo ilianzishwa mwaka 2001 na nchi nne za Brazil, Russia, China na India ambazo uchumi wao ulikuwa unastawi kwa kasi kubwa na kisha Afrika Kusini kujiunga nayo miaka michache baadaye. Safari hiyo ya rais wa China katika nchi zilizotajwa za Kiafrika na Kiarabu ina umuhimu mkubwa kwa kutilia maanani kwamba inafanyika katika mazingira ambayo kiwango cha bidhaa za China zinazoingizwa nchini Marekani kimepungua sana kutokana na hatua ya serikali ya Rais Doland Trump  wa nchi hiyo kuziongezea ushuru mkubwa bidhaa hizo.

Rais Xi Jinping akikaribishwa nchini Tanzania katika safari zake za huko nyuma barani Afrika

China ambayo katika miaka iliyopita imewekeza pakubwa katika nchi za Kiafrika hivi sasa inafanya juhudi za kizitafutia soko bidhaa zake katika bara hilo. Baada ya kupungua kiwango cha uuzaji wa bidhaa zake nchini Marekani sasa China inafanya juhudi za kuzitafutia bidhaa hizo soko jingine hususan katika nchi za Kiarabu na Kiafrika. Ili kuvitafutia malighafi viwanda vyake, China inalitazama bara la Afrika kama mdhamini thabiti na rahisi wa malighafi hizo. Mbali na suala hilo, vyanzo vya nishati vinavyotambulika barani Afrika ni mojawapo ya njia za kudhamini mahitaji ya nishati ya viwanda vya China ambayo kasi kubwa ya kustawi uchumi wake imeifanya serikali ya Beijing kuwa moja ya wanunuzi na watumiaji wakubwa wa nishati duniani. Uwekezaji mkubwa ambao umefanywa na China katika sekta ya mafuta ya Sudan katika miaka ya hivi karibuni, ni moja ya mifano inayothibitisha kwamba Beijing inatafuta njia tofauti za kujidhaminia nishati kupitia ushirikiano na wazalishaji nishati katika fremu ya kudhamini uwekezaji na kuhamishwa teknolojia.

Nchi wanachama wa BRICS

Kuhusiana na suala hilo jarida la Global Times limeandika kwamba utendaji wa China katika nchi za Kiafrika na hasa nchini Sudan unaonyesha kuwa nchi hiyo ya Asia  katika miongo kadhaa iliyopita imeweza kubuni mfumo mpya wa kiuchumi kwa ajili ya kushirikiana na nchi za Kiafrika. Kwa mtazamo huo Rais Jinping amefanya safari katika nchi tano zilizotajwa za Kiarabu na Kiafrika ili kutia saini mikataba mpya ya ushirikiano na kuimarisha miamala ya kiuchumi ya pande mbili. Tunapaswa pia kutilia maanani kwamba katika miaka ya hivi karibuni bara la Afrika limegeuka na kuwa uwanja wa mashindano makali ya kiuchumi kati ya China na Marekani na kuhusiana na hilo China inaonekana kuishinda Marekani katika uwanja huo kwa kuwekeza dola bilioni moja kwa mwaka barani humo. Moja ya mambo ambayo yamezifanya nchi nyingi za Afrika kuvutiwa na China ikilinganishwa na Marekani, ni mpango wa nchi hiyo ya Asia wa kutoa msaada wa kiuchumi na kuwekeza barani humo bila ya kushurutisha uwekezaji huo na masuala ya kisiasa.

Mashindano makali ya kibiashara na kiuchumi ya Marekani na China barani Afrika

Kuhusu hilo jarida la Global Times linaendelea kuandika kwamba uwekezaji wa kiuchumi wa China na ushiriki wake katika miradi mikubwa ya miundombinu katika bara hilo haujafungamanishwa na masuala yoyote ya kisiasa wala kutwishwa nchi za bara hilo mambo zisizokubaliana nayo. Ni katika mazingira hayo ndipo safari ya hivi sasa ya Rais Xi Jinping katika nchi tano za Kiarabu na Kiafrika ikachuliwa kuwa itakayokuwa na mafanikio makubwa.

Jul 21, 2018 01:18 UTC
Maoni