• Ripoti: Uingereza inawatumia watoto kama majasusi

Ripoti mpya ya Bunge la Uingereza imefichukua kuwa, polisi na idara za kijasusi nchini humo zinawatumia watoto wadogo katika operesheni hatarishi za kijasusi.

Ripoti hiyo iliyochapishwa na kamati ya Bunge la Juu la Uingereza (House of Lords) imebainisha kuwa, idara ya polisi na za kiitelijensia zinawatumia watoto wadogo wenye chini ya umri wa miaka 16 katika operesheni za kijasusi, dhidi ya magaidi, magenge ya uhalifu na walanguzi wa mihadarati.

Mwenyekiti wa kamati hiyo David Trefgarne amesema, "Tuna wasiwasi mkubwa kutokana na mwenendo huo wa kuwatumia watoto wadogo katika operesheni hizo hatari za kupambana na jinai, na iwapo watoto hao wataendelea kutumiwa kwa muda mrefu katika operesheni hizo, tunawaweka katika hatari ya kukumbwa na matatizo ya kisaikolojia na kimwili."

Mtoto wa Kimagharibi na bastola mkononi

Hata hivyo ripoti hiyo haijaweka wazi idadi ya watoto waliotumika kufikia sasa katika operesheni za kukusanya taarifa za kijasusi kwa niaba ya vyombo vya usalama nchini Uingereza.

Shirika la kutetea haki za binadamu la Rights Watch UK limeeleza kusikitishwa kwake na ripoti hiyo, na kusema kuwa, chini ya sheria za kitaifa na kimataifa, maamuzi yoyote yanayowahusu watoto yanapaswa kuwa yenye maslahi mapana kwao na sio vinginevyo.

 

Tags

Jul 21, 2018 01:19 UTC
Maoni