Aug 14, 2018 02:53 UTC
  • Waislamu Uingereza wataka hatua kali zichukuliwe dhidi ya Boris Johnson

Waislamu wa Uingereza wametaka uchunguzi kamili ufanyika kuhusu waziri wa zamani wa mambo ya nje wa nchi hiyo, Boris Johnson ambaye amewakashifu Waislamu.

Baraza la Waislamu wa Uingereza ambayo inahesabiwa kuwa ndiyo taasisi kubwa zaidi ya Waislamu nchini humo, limemwandikia barua Waziri Mkuu Theresa May likitaka kufanyika uchunguzi wa kina kuhusu Johnson kwa matamshi yake ya kuwakashifu wanawake wa Kiislamu.

Wajumbe wa Baraza la Waislamu wa Uingereza wamesema katika barua hiyo kwamba haipasi kuruhusu jamii za wachache zifanywe wahanga.

Boris Johnson, waziri wa mambo ya nje wa Uingereza aliyewatukana Waislamu kutafuta umaarufu

 

Baraza hilo limeongeza kuwa, tangu ilipochapishwa makala ambayo ndani yake Boris Johnson aliwadhalilisha na kuwatukana wanawake wa Kiislamu, vitendo vya chuki na ukandamizaji dhidi ya Waislamu wa Uingereza navyo vimeongezeka sana.

Hivi karibuni gazeti la Dily Telegraph lilichapisha makala ya waziri huyo wa zamani wa mambo ya nje wa Uingereza akidai kuwa wanawake wa Kiislamu wanaovaa burqa na niqabu ni sawa na wezi wa mabenki na visanduku vya posta.

Hadi sasa hakuna hatua yoyote ya maana iliyochukuliwa dhidi ya mtukanaji huyo wa Waislamu licha ya kuwasilishwa makumi ya mashtaka dhidi yake.

Wakati huo huo taasisi ya Tell Mama ambayo inachunguza na kurekodi mashambulizi ya kibaguzi nchini Uingereza nayo imesema kuwa, vitendo vya chuki na udhalilishaji dhidi ya Waislamu wanaovaa vazi la staha la Hijab vimeongezeka sana nchini Uingereza tangu ilipochapishwa na kusambazwa makala hiyo ya kuwakashifu Waislamu. 

Tags

Maoni