Aug 15, 2018 07:39 UTC
  • Mzozo wa Marekani na Uturuki wakolea, bidhaa za Marekani zapigwa marufuku kutangazwa nchini humo

Mashirika kadhaa ya Uturuki yametangaza kwamba kuanzia sasa hayatokubali kutangaza bidhaa za Marekani kama ambavyo pia hayatotoa idhini kwa mashirika ya Marekani kutangaza bidhaa zake ndani ya nchi hiyo.

Mashirika hayo likiwemo shirika la Telecom na shirika la ndege la Uturuki la THY yamesisitiza hayo katika kampeni iliyopewa jina la 'Usiipe Marekani fursa ya kutangaza biashara' na kusema kuwa, yatasimama pamoja na serikali na taifa kwa ajili ya kukabiliana na Marekani. Aidha mashirika hayo yamezitaka taasisi na mashirika yote ya Uturuki kujiunga na kampeni hiyo. Ijumaa iliyopita, rais Donald Trump wa Marekani alizipandishia ushuru wa forodha kwa mara mbili zaidi bidhaa za chuma na aluminiamu za Uturuki.

Mvutano unaoendelea kati ya Uturuki na Marekani

Aidha tarehe Mosi mwezi huu na kufuatia hatua ya serikali ya Ankara ya kukataa kumuachilia huru, Adrew Brunson, padri wa Kimarekani anayeendelea kushikiliwa nchini Uturuki kwa tuhuma za ujasusi na ugaidi, Washington iliwawekea vikwazo mawaziri wawili wa mambo ya ndani na sheria wa Uturuki. Hatua hizo za Marekani zimepelekea kuporomoka kwa karibu asilimia 35 thamani ya sarafu ya Lira, ambayo ni pesa ya Uturuki mkabala wa Dola ya Marekani. Waturuki hususan wafuasi wa Rais Recep Tayyip Erdoğan, wanaamini kwamba, mgogoro wa fedha nchini humo unatokana na njama za Marekani kwa ajili ya kuidhoofisha Uturuki. Wakati huo huo, Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki ametangaza Jumanne ya jana kuwekewa vikwazo bidhaa za kielektroniki zinazozalishwa nchini Marekani.

Maoni