Aug 16, 2018 13:27 UTC
  • Korea Kaskazini yaitaka Korea Kusini kutoifuata Marekani katika vikwazo vipya

Siku moja baada ya Wizara ya Hazina ya Marekani kuyawekea vikwazo mashirika matatu ya meli za kigeni ya Korea Kaskazini, serikali ya Pyongyang imeitaka Korea Kusini kutoshirikiana na Marekani katika vikwazo hivyo.

Gazeti rasmi la serikali ya Korea Kaskazini la Rodong Sinmun limeandika leo kwamba, juhudi za Korea Kusini za kuzidisha mashinikizo na vikwazo dhidi ya Pyongyang, zinakwenda kinyume na nara ya kustawisha uhusiano na Korea Kaskazini. Gazeti hilo pia limewanukuu viongozi wa ngazi ya juu wa Korea Kaskazini wakionya kwamba, iwapo Korea Kusini itafuata kibubusa vikwazo vya Marekani dhidi yake, basi uhusiano wa nchi mbili ambao ni kwa maslahi ya raia utakabiliwa na hali ngumu.

Mkutano wa Trump na Kim Jong-un huko Singapore haukuwa na faida yoyote

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Marekani inaingilia kwa njia isiyo ya moja kwa moja katika masuala ya ndani ya Korea Kaskazini kama ambavyo inaingilia pia katika uhusiano kati ya Pyongyang na Seoul na hivyo kuzuia kufikiwa maridhiano, umoja na mazungumzo na ushirikiano kati ya Korea mbili. Jana usiku Wizara ya Hazina ya Marekani, ilitangaza kuyawekea vikwazo mashirika matatu ya meli za kigeni kutoka China, Russia na Singapore ambazo zimekuwa zikipeleka bidhaa mbalimbali huko Korea Kaskazini.

Vikwazo hivyo vimewekwa katika hali ambayo Kim Jong-un Kiongozi wa Korea Kaskazini na Rais Donald Trump wa Marekani walikutana tarehe 12 Juni mwaka huu nchini Singapore na kutiliana saini makubalianoa ambayo kwa mujibu wake Pyongyang iliahidi kuangamiza silaha zake za nyuklia na mkabala wake Marekani kuidhamini usalama nchi hiyo.

Maoni