Aug 17, 2018 04:41 UTC
  • Pentagon: China inajitayarisha kuishambulia Marekani

Ripoti iliyotolewa na Wizara ya Ulinzi ya Marekani, Pentagon imesema kuwa jeshi la China limepanua operesheni za ndege zake za kivita katika miaka ya hivi karibuni na kwamba kuna uwezekano kwamba zinafanya mazoezi ya kufanya mashambulizi dhidi ya Marekani na waitifaki wake.

Taarifa ya Pentagon ambayo imetolewa wakati huu ambapo nchi hizo mbili ziko katika mvutano mkubwa unaohusiana na vita vya kiuchumi vya Donald Trump, imeashiria kile ilichokiita juhudi za China za kuongeza ushawishi wake wa kimataifa, na matumizi ya ulinzi ambayo Pentagon inakadiria kuwa yamezidi dola bilioni 190 mwaka 2017.

Ripoti ya Wizara ya Ulinzi ya Marekani imeongeza kuwa: "Kwa zaidi ya miaka mitatu iliyopita, Jeshi la Ukombozi la Watu wa China (PLA) limezidi kupanua maeneo ya operesheni za ndege za kijeshi baharini na kupata uzoefu katika maeneo muhimu ya baharini, na kuna uwezekano kwamba linafanya mazoezi ya jinsi ya kuishambulia Marekani na waitifaki wake."

Jeshi la China.

Ripoti hiyo imetolewa wakati nchi mbili za China na Marekani zinajitayarisha kufanya mazungumzo juu ya jinsi ya kutatua hitilafu za pande mbili kuhusu ushuru wa forodha.

Vita vya kibiashara baina ya pande hizo mbili vilianza baada ya Rais Donald Trump wa Marekani kuzidisha ushuru wa forodha kwa bidhaa za China zinazoingizwa nchini Marekani ambapo China ilirudisha mapigo kwa kupandisha ushuru wa forodha kwa bidhaa za Marekani.

Katika stratejia yake mpya ya usalama wa taifa, Washington imeitaja China na Russia kuwa ni adui na tishio kubwa kwa Marekani.

Tags

Maoni