• London yakataa matakwa ya Marekani ya kuiwekea vikwazo Iran

Wizara ya Mambo ya Nje ya Uingereza imekataa wito wa Marekani wa kujiunga na Washington katika vikwazo vyake vipya dhidi ya Iran.

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Uingereza imetilia mkazo udharura wa kuheshimiwa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA baina ya nchi 5 wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na Ujerumani kwa upande mmoja na Iran katika upande mwingine na kusema kuwa, makubaliano hayo yana umuhimu mkubwa kwa ajili ya kulinda usalama wa Mashariki ya Kati. 

Marekani imekuwa ikiwataka maafisa wa serikali ya Uingereza kufuata nyayo za Washington katika vikwazo vyake vipya dhidi ya Iran na kutahadharisha kuwa, makampuni ya Uingereza ambayo yataendeleza biashara na Iran yataadhibiwa na Washington. Marekani pia imetishia kuyachukulia hatua na kuyaadhibu makampuni ya nchi nyingine yoyote itakayofanya biashara na Iran. 

Licha ya upinzani wa nchi mbalimbali duniani dhidi ya siasa zake za mabavu na kupenda makuu, Marekani imeanzisha vita vya kinafsi inavyotumia kuzitisha nchi na makampuni makubwa ya biashara kwa shabaha ya kuyalazimisha yafuate nyayo zake katika vikwazo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu. Hata hivyo Umoja wa Ulaya na nchi wanachama katika umoja huo na vilevile nchi kama Russia, China, Pakistan, Uturuki na India zimetangaza kuwa, hazitajiunga na Marekani katika vikwazo vyake vipya dhidi ya Iran kwa sababu suala hilo linapingana na maslahi yao ya kitaifa. Umoja wa Ulaya unataka kubakisha hai na kulinda makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na unayatambua kuwa ni matunda makubwa katika mtazamo wa kiusalama. Sambamba na kuanza kutekelezwa vikwazo vipya vya Marekani dhidi ya Iran umoja huo umehuisha tena sheria inayoyaadhibu makampuni ya Ulaya yatakayofuata nyayo za Marekani dhidi ya Iran.

Umoja wa Ulaya na nchi nyingine kadhaa duniani zinafanya jitihada za kulinda maslahi yao ya kitaifa na zimetangaza waziwazi kwamba, makubaliano ya nyuklia ya JCPOA ni matunda muhimu ya kimataifa yanayodhamini maslahi yao ya kiuchumi, kisiasa na kiusalama. 

Dunia inapinga vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran

Hatua ya Umoja wa Ulaya ya kuhuisha tena sheria hiyo imezidisha mivutano kati ya Marekani na washirika wake wa Ulaya. Hata hivyo inatupasa kusema kuwa, sera za kujichukulia maamuzi ya upande mmoja na kupuuza maslahi ya nchi nyingine za Marekani pia zinazidisha ufa na hitilafu kati ya pande mbili za Bahari ya Atlantic. Peter Harrell ambaye ni mtaalamu wa Center for a New American Security anasema kuwa: Marekani itakabiliwa na matatizo katika jitihada zake za kutaka kuzishawishi nchi nyingine zikate uhusiano wao wa kibiashara na Iran kwa sababu ya kukiuka kwake makubaliano ya kimataifa ya JCPOA.

Upinzani wa wazi wa watifaki wakubwa zaidi wa Marekani dhidi ya vikwazo vipya vya nchi hiyo ni ishara ya kuendelea kutengwa serikali ya Washington katika masuala ya kimataifa, suala ambalo linaweza kuhesabiwa kuwa ni mafanikio ya Iran katika upeo wa kimataifa.  

Tags

Aug 17, 2018 07:11 UTC
Maoni