Aug 24, 2018 02:43 UTC
  • Changamoto mpya zamkumba Rais Trump wa Marekani

Tokea wakati Rais Donald Trump wa Marekani alipoingia madarakani hadi sasa, amekumbwa na changamoto nyingi ndani ya nchi. Moja ya changamoto hizo ni tuhuma kuwa Russia ilihusika katika kuingilia mchakato wa uchaguzi wa rais wa Marekani mwaka 2016 kwa maslahi ya Trump.

Uchunguzi kuhusu kadhia hiyo ya Russia ungali unaendelea na hivyo Trump bado hajaweza kujua hatima ya uchunguzi huo. Lakini changamoto mpya ambayo Trump anakumbana nayo sasa ni kupatikana na hatia wafanyakazi wake wa zamani na sasa kuna uwezekano mkubwa wa kusailiwa na kuuzuliwa mtawala huyo wa Marekani.

Trump ametoa radiamali yake baada ya kusikilizwa kesi na kupatikana na hatia wakili wake wa zamani  Michael Cohen na mkuu wa zamani wa idara yake ya kampeni Paul Manafort na sasa kuna uwezekano mkubwa wa kusailiwa na kuuzuliwa mtawala huyo wa Marekani kabla ya kukamilisha kipindi chake cha urais. Siku ya Jumanne mahakama ilimpata Manafort na hatia nane huku Cohen naye akikiri makosa ya kukiuka sheria za fedha za kampeni katika uchaguzi wa rais mwaka 2016. Kile kilicho na umuhimu katika kukiri huko ni kuwa Cohen anasema alikiuka sheria kwa idhini ya Trump na kwa lengo la kubadilisha matokeo ya uchaguzi wa rais wa Marekani.

Katika radiamali yake ya awali kupitia ujumbe wa Twitter, Jumatano, Trump sambamba na kumsifu Manafort kuwa ni mtu shujaa aliongeza kuwa: "Iwapo mtu anataka wakili mzuri, na mshauri asimchukue Michael." Kuhusu Manafort Trump ameandika: "Mahakama imechukua kesi ya ushuru ya miaka 12 iliyopita kati ya mengine na kumshinikiza sana Manafort."

Hata kama Trump hana uhusiano na makosa ambayo Manafort amepatikana na hatia ya kuyatenda lakini jambo hilo litakuwa na taathira mbaya kwa rais huyo wa Marekani.

Cohen naye amepatikana na hatia ya makosa matano ya kukwepa kulipa kodi, kukiuka sheria za kifedha za uchaguzi na utapeli wa kibenki. Faili la Cohen pia ni sehemu ya uchunguzi unaofanywa na Robert Mueller, mkuu wa jopo maalumu linalofanya uchunguzi kuhusu madai ya kuhusika Russia katika kubadilisha matokeo ya uchaguzi wa mwaka 2016 kwa maslahi ya Trump. Cohen amekiri kuwa alimlipa kitita cha fedha mcheza filamu za ngono ili anyamaze kimya kuhusu uhusiano wake wa kingono na Trump.

Adam Schiff, mbunge wa chama cha Demokrat ambaye ni mwanachama wa ngazi za juu wa kamati ya intelijensia katika Bunge la Senate la Marekani anasema: "Matamshi ya Michael Cohen kuhusu kukwepa kulipa kodi, utapeli wa kibenki na ukiukwaji wa sheria za kifedha zinazohusu kampeni za uchaguzi ikiwa ni pamoja na kumhonga mwanamke aliyekuwa na uhusiano wa kingono na Trump ili anyamaze kimya ni sehemu nyingine ya kukiri makosa watu walio karibu na Trump. Kuhusishwa rais na ukiukwaji wa sheria za kifedha katika kampeni za uchaguzi ni jambo ambalo litapelekea Trump akumbwe na matatizo ya kisheria.

Bunge la Marekani

Hivi sasa Trump anakabiliwa na mustakabali wenye kiza na ndio sababu rais huyo akaamua kunyamaza kimya kuhusu jinai ambazo Cohen amekiri kuzitenda. Kuna uwezekano kuwa Cohen bado ana siri nyingi kuhusu kampeni za Trump ambazo anapanga kumpa Mueller. Wakuu wa idara za kijasusi za Marekani wanaamini kuwa Russia iliingilia uchaguzi wa rais wa nchi hiyo kwa maslahi ya Trump na hivyo kumsaidia kupata ushindi. Trump amekanusha madai hayo na Russia pia imekanusha kuingilia uchaguzi wa Marekani. Kwa kuzingatia uwezekano mkubwa wa Wademocrat kupata ushindi katika uchaguzi wa bunge wa Novemba 6 mwaka huu, yamkini Trump akasailiwa na hatimaye kuuzuliwa kabla ya muhula wake kumalizika. 

Tags

Maoni